Wiki iliyopita klabu ya soka ya jiji la Kampala nchini Uganda KCCA ilitawazwa bingwa wa ligi kuu ya soka nchini humo msimu huu.
KCCA FC ilipata taji lake la 11 katika historia yake ya ligi kuu nchini humo, tangu mwaka 1976 ilipopata taji lake la kwanza.
Huu ndio ubingwa wa kwanza wa kocha Mike Mutebi ambaye amekuwa akifunza soka nchini humo kwa miaka 20 sasa.
Mutebi anasema kitu kilichomsaidia kunyakua ubingwa ni kuwatumia wachezaji chipukizi wote kutoka nchini Uganda.
Aidha, amesema hana mpango wa kuwasajili wachezaji kutoka nje ya nchi hata wale wa nchi jirani.
Soka25east.com imezungumza na kocha Mutebi akiwa jijini Kampala.
Soka25east.com: Kocha Mutebi asante sana kwa kuzungumza nasi ukiwa hapo jijini Kampala.
Kocha Mutebi: Asante sana.
Soka25east.com:Hongera sana kwa ushindi uliopata na klabu yako ya KCCA, tuambie siri ya mafanikio ni nini ?
Kocha Mutebi: Aaaa..tulikuwa na vijana wadogo, wenye umri wa chini ya miaka 23. Ulikuwa ni msimu wao wa kwanza kucheza ligi kuu hapa Uganda. Hakika walicheza kwa moyo. Walijtolea sana.
Soka25east.com: Ni hilo tu ?
Kocha Mutebi: Kuna utofauti mkubwa katika klabu hii na vlabu vingine hapa Uganda.Mazingira ya kufanya kazi ni mazuri sana.Mimi kocha nilipewa nafasi ya kipekee kufanya kazi yangu bila ya kuingiliwa na yeyote.
Soka25east.com: Baada ya ubingwa huu, una mpango wa kubadilisha kikosi chako msimu ujao ?
Kocha Mutebi: Tuna vijana wadogo lakini tutawatafuta wachezaji wengine wenye uzuri kutoka hapa nchini Uganda, lakini sio kutoka nje ya Uganda hatuwezi kwenda Afrika Mashariki, Tanzania …hapana…tutasalia hapa Uganda.
Soka25east.com: Kwanini Kocha ?
Kocha Mutebi: Umeona wachezaji wa Uganda wakiichezea klabu ya Simba, Yanga na Al Merrikh. Hii inaonesha kuwa wachezaji wa Uganda ni wazuri sana kwa kweli. Lakini hata kama tungependa kutafuta mshambuliaji namba 9 kutoka Afrika Magharibi, je tuna Dola Milioni 1 kumnunua ? Hatuna hizo pesa kwa hivyo tutawatumia tu wachezaji wetu hapa Uganda.
Soka25east.com: Mwaka ujao KCCA itashiriki katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika, matarajio yako ni yepi ?
Kocha Mutebi: Lengo letu ni kufika katika hatua ya makundi.Tuna kikosi kizuri na sina shaka kuwa tunaweza kufanya vizuri na tutacheza kwa bidii. Hili ndilo lengo letu.
Soka25east.com: Asante sana kocha Mutebi kwa kuzungumza nasi ukiwa hapo Kampala, bila shaka unaendelea kusherehekea na wachezaji wako. Kila la heri.
Kocha Mutebi: Asante sana.