Shirikisho la soka nchini Uganda, FUFA, limekanusha madai kuwa halijalipa marupurupu ya wachezaji wa timu ya taifa na viongozi wa kiufundi wa timu hiyo.
Mkurugenzi wa fedha Decolas Kizza amesema Shirikisho hilo limelipa kiasi kikubwa cha marupurupu hayo na kinachosalia ni kiasi kidogo tu.
Aidha, ameongeza kuwa FUFA haitaweka wazi kiasi cha fedha ambacho hakijalipwa lakini pia ni mechi zipi ambazo wachezaji hawakupokea marupurupu yao.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa marupurupu yote yatakamilishwa kwa wachezaji na wakuu wa kiufundi kabla ya mchuano dhidi ya Comoris kufuzu kucheza fainali ya bara Afrika mwezi Septemba.
Ripoti za awali, zilidai kuwa wachezaji pamoja na benchi lote la kiufundi akiwemo kocha Milutin Micho hawajalipwa baada ya kushiriki katika michuano kadhaa za kimataifa.
FUFA inasema ikiwa, Uganda Cranes wataishinda Comoros wataongezewa Dola 500 za Marekani katika Dola 2000 wanazolipwa baada ya kila mechi.
Uganda inatafuta kwa udi na uvumbi kufuzu katika michuano ya mataifa bingwa barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1978.