Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya soka ya Cameroon Paul Le Guen amesema hatachukua nafasi ya kuwa mshauri wa kiufundi wa timu ya taifa ya soka ya Nigeria.
Hili limebainika baada ya Shirikisho la soka wiki hii kutangaza katika nafasi hiyo ili kushirikiana na kocha Mkuu Salisu Yusuf kuiongoza timu hiyo.
Hata hivyo, NFF imeliambia Shirika la Habari la Uingereza BBC kuwa wao kama Shirikisho wameshindwa kukubaliana na Guen kuhusu maswala ya mkataba.
Aidha, ripoti zinasema kuwa ni kweli kocha huyo alikuwa katika mazungumzo na uongozi wa soka nchini Nigeria lakini hakuna mwafaka uliopatikana.
Kwa sasa Yusuf anaendelea kuiongoza Super Eagles na mchuano wake wa kwanza ulikuwa ni wa kimataifa wa kirafiki kati ya Mali na Luxembourg na kupata ushindi.
Nigeria ilishindwa kufuzu katika michezo ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2017 itakayofanyika nchini Gabon lakini ipo katika harakati za kutafuta tiketi ya kufuzu katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Nigeria imewekwa katika kundi moja na Algeria, Cameroon na Zambia.