Connect with us

 

Mashabiki na wadau wa soka Afrika Mashariki wanaomboleza kifo cha kocha wa muda mrefu na kipa wa zamani wa Timu ya taifa ya Kenya, James Siang’a.

Siang’a, alifariki dunia siku ya Ijumaa usiku akiwa na umri wa miaka 67 akiwa hospitalini mjini Bungoma baada ya kusumbuliwa muda mrefu na ugonjwa wa kisukari.

Rais wa Shirikisho la soka nchini Kenya Nick Mwendwa, mwenzake wa Tanzania Jamal Malinzi, Katibu Mkuu wa Baraza la soka Afrika Mashariki CECAFA Nicholas Musonye na kocha wa timu ya taifa ya soka ya Uganda Milutin “Micho” Sredojevic, ni miongoni mwa wadau wa soka waliomkumbuka kocha Siang’a aliyesaidia kuinua soka Afrika Mashariki.

Atakumbukwa sana nchini Kenya kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa timu ya taifa na klabu ya Gor Mahia na timu ya taifa miaka ya 60 na 70.

Licha ya kuichezea Kenya, Siang’a alikuwa kocha wa timu ya taifa Harambee Stars kati ya mwaka 1999-2000 kabla ya kwenda nchini Tanzania na kuifunza klabu ya Simba FC kati ya mwaka 2001-2003.

Wakati akiifunza klabu ya Simba, aliifikisha klabu hiyo katika hatua ya makundi kuwania taji la klabu bingwa na kuwashinda mabingwa watetezi wakati huo Zamalek FC.

Aidha, wakati akiifunza klabvu ya Simba mwaka 2002 aliiongoza kushinda taji la klabu bingwa Afrika Mashariki CECAFA.

Haya ni mafanikio ambayo mashabiki wa klabu ya soka nchini Tanzania bado wanayakumbuka hadi leo.

Akiwa pia nchini Tanzania, aliifunza timu ya taifa ya soka Taifa Stars mwaka huo wa 2002.

Baada ya kuondoka nchini Tanzania, kati ya mwaka 2003 na 2004, alikwenda nchii Uganda kuifuza klabu ya Express FC lakini baadaye mwaka huo akarejea tena nchini Tanzania kuifunza Moro United kati ya mwaka 2004 na 2005 na Mtibwa Sugar kwa 2007.

Baadaye alirudi nyumbani na mwaka 2009, aliifunza klabu ya Gor Mahia ambayo wakati huo ilikuwa inafanya vibaya na kuisaidia kupata wachezaji chipukizi walioisaidia klabu hiyo kushinda ligi mara tatu mfululizo mwaka 2013, 2014 na 2015.

More in