Na Victor Abuso,
Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars imeanza vibaya michuano ya kuwania ubingwa wa soka baina ya mataifa ya Kusini mwa Afrika inayoendelea nchini Afrika Kusini baada ya kufungwa na Swaziland bao 1 kwa 0.
Swaziland ambao wanaorodheswa chini ya Tanzania katika orodha ya mataifa bora ya Shirikisho la soka duniani FIFA waliwashangaza mashabiki kwa kupata ushindi huo muhimu kupitia bao la mchezaji Sifiso Mabila.
Timu hizi mbili zilikutana mara ya mwisho mwaka uliopita katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki na kutoka sare ya kufungana bao 1 kwa 1.
Taifa Stars ambayo imealikwa katika michuano hiyo sasa ina kazi kubwa kesho Jumatano katika mchuano wake dhidi ya Madagascar ili kuwa na matumaini ya kusonga mbele.
Baadhi ya mashabiki wa Taifa Stars jijini Dar es salaam wanasema hawaoni timu yao ikifika mbali kwa kile wanachokisema kuwa kocha Mart Nooij hakukiteua kikosi sahihi kushiriki katika michuano hii.
‘Kwa kweli niliuona mchuano huo, sisi tulifanikiwa tu kulenga golini mara tatu kinyume na Swaziland ambao walikuwa wametulia,” alisema Emmanuel Richard mkaazi wa Dar es salaam.
“Sioni tukifika mbali tukiendelea kucheza kama ilivyokuwa jana,” aliongeza.
Mbali na Tanzania, katika matokeo mengine ya michuano hiyo Jumanne usiku, Madagascar walitoka nyuma na kuwashinda Lesotho mabao 2 kwa 1.
Madagascar wanaongoza kundi la B kwa alama 3 wakifuatwa na Swaziland huku Lesotho na Tanzania zikikosa alama.
Siku ya Jumanne usiku michuano ya kundi la A, zitarejelewa na Ushelisheli wanamenyana na Zimbabwe kuanzia saa kumi na mbili kamili jioni saa za Afrika Mashariki lakini baadaye saa mbili na nusu usiku Namibia watamenyana na Mauritius.
Mshindi katika kila kundi atafuzu katika hatua ya robo fainali.