Connect with us

Ulinzi Stars imeondolewa katika michuano ya Shirikisho barani Afrika licha ya kupata ushindi wa mabao 3-0 nyumbani katika mchuano wa marudiano dhidi ya Smouha ya Misri siku ya Jumamosi.

Timu hii ya jeshi la Kenya ikicheza katika uwanja wa Kenyatta mjini  Machakos, ilionesha mchezo wa hali ya juu lakini kwa sababu ilikuwa imefungwa mabao 4-0 katika mchuano wa mzunguko wa kwanza nchini Misri, walihitaji ushindi wa angalau mabao 5-0 ili kusonga mbele.

Licha ya kuondolewa kwa jumla ya mabao 4-3, Ulinzi Stars walianza kipindi cha kwanza kwa kushambulia lango la wapinzani wao na kupata bao la kwanza kupitia Sammy Onyango,  dakika ya 10 ya mchuano huo.

Ulinzi Stars yenye makao yake mjini Nakuru, iliendeleza kasi ya mchezo na muda mfupi kabla ya wakati wa mapumziko, Sammy Onyango alifunga timu yake bao la pili.

Kipindi cha pili, vijana wa kocha Benjamin Onyango waliendeleza mashambulizi lakini beki ya Smouha ilionekana kuwa imara, na ilipofika dakika ya 55, klabu hiyo ilibaki na wachezaji 10 baada ya Kago kupata kadi nyekundu na kuondolewa uwanjani.

Dakika 20 kabla ya kumalizika kwa mchuano huo, Omar Bongi aliifungia klabu yake bao la 3.

Matokeo mabaya ugenini kwa mara nyingine, yameondosha klabu ya Kenya katika michuano hii mikubwa barani Afrika.

Kikosi cha Ulinzi : James Saruni, Brian Birgen, Godfrey Kokoyo, Mohammed Hassan, Omar Mbongi, Boniface Onyango, Churchill Muloma, John Kago, Samuel Onyango, Evans Amwoka, Daniel Waweru

Wachezaji wa akiba: Finus Odhiambo, Benson Sande, Oliver Rutto, Enosh Ochieng, Oscar Wamalwa, Justine Omwonga, Baron Oketch

More in