Na Victor Abuso,
Viongozi wa Shirikisho la soka Afrika Mashariki na Kati wapo njiani kwenda kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Shirikisho la soka mjini Zurich nchini Uswizi kushiriki katika uchaguzi wa urais wa FIFA siku ya Ijumaa.
Ushindani ni kati ya rais wa sasa Sepp Blatter na Mwanamfalme wa Jordan Ali Bin Al-Hussein baada ya wagombea wengine akiwemo Michael Van Praag rais wa Shirikisho la soka nchini Uholanzi na mchezaji wa zamani wa Ureno Louis Figo kujiondoa katika dakika za lala salama.
Leodegar Tenga rais wa Shirikisho la soka Afrika Mashariki na Kati CECAFA tayari ametangaza kuwa viongozi wa eneo hilo watampigia kura Sepp Blatter, kauli iliyoafikiwa wakati walipokutana jijini Nairobi nchini Kenya hivi karibuni.
CECAFA inasema Blatter amekuwa katika mstari wa mbele kusaidia kuinua soka katika eneo hilo na hivyo hawana kingine ila kumpigia kura ili kuendelea kuongoza.
Anthony Aroshee, mchambuzi wa soka akiwa mjini Mombasa nchini Kenya anaona kuwa ni wazi Blatter ataibuka mshindi kwa sababu viongozi wa bara la Afrika wameonesha nia ya kumuunga mkono na wanamkubali.
“ Unajua ukipata kura zote za Afrika, unakuwa katika nafasi nzuri ya kushinda wadhifa huu.Kwa hivyo sioni ni kwanini “Babu” Blatter asishinde,” aliongezea Aroshee.
Tayari FIFA imesema kuwa itatumia Euro Milioni 600,000 kufanikisha safari na malazi ya viongozi wa soka barani Afrika wapatao 54 pamoja na wengine duniani.
Jumla ya mashirikisho ya soka duniani 209
Ulaya (Uefa) 53
Afrika (Caf) 54
Asia (AFC) 46
Kaskazini & America ya Kati 35
Oceania (OFC) 11
Marekani Kusini 10