Na Victor Abuso,
Shirikisho la soka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Fecofa) limetangaza kuwa michuano ya kuwania taji la taifa ya Congo litachezwa kati ya tarehe 10 mwezi Juni hadi tarehe 23 mwaka huu.
Ratiba hiyo inaeleza kuwa michuano ya makundi itachezwa kati ya tarehe 10 hadi 14 mjini Lubumbashi, jijini Kinshasa na mjini Bukavu.
Wizara ya michezo nchini humo ilitoa siku 25 kwa kuchezwa kwa michuano hiyo baada ya kuzuka kwa tofauti kuhusu mwandalizi wa michuano hii kati ya chama cha soka Fecofa na wasimamizi wa michuano hii Linafoot .
Michuano hii huandaliwa baada ya kukamilika kwa ligi kuu ya soka nchini humo ambayo msimu huu klabu ya Vita Club imeibuka bingwa kwa alama 21, ikifuatwa na TP Mazembe kwa alama 20 huku Don Bosco ikiwa ya tatu kwa alama 15.
Vlabu vinavyotaka kushiriki katika michuano hii vitahitajika kulipa Dola za Marekani 500 na vile vinavyotaka kushiriki vimepewa saa 72 kuwasilisha maombi yao kwa chama cha soka Fecofa.
FC MK Étanchéité ndio mabingwa watetezi wa taji hili.