Na Victor Abuso,
Hatua ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa klabu ya AFC Leopards Allan Kasavuli kwa sababu za changamoto za kifedha sio suluhu ya kumaliza masaibu ya klabu hii kongwe nchini Kenya na katika eneo la Afrika Mashariki.
Ukweli ni kwamba na kama alivyosema Kasavuli mwenyewe wakati akijiuzulu, ukosefu wa fedha baada ya kujiondoa kwa mfadhili Mumias Sugar hakika ilikuwa ni pigo kubwa kwa uongozi wa klabu hiyo.
Kwa mtazamo wangu, nafikiri tatizo kubwa la AFC Leopards sio ukosefu wa ufadhili bali ni siasa mbaya ndani ya klabu hiyo.Ndio siasa.
Kuna wale wenye mawazo finyu kuwa mtu asiyetokea eneo la Magharibi au yeyote ambaye sio Mluhya hastahili kuongoza klabu hiyo.Wengine wamesikika wakisema, “AFC Leopards ni yetu”.
Inasikitisha kusikia upande pinzani wa uongozi wa klabu hiyo unaoongozwa na Mathews Opwora aliyehojiwa na tovuti ya michezo ya Goal.com akisema kuwa wao hawatambui kamati ya mpito inayoongozwa na Alex Ole Magelo. Kama hii si siasa, ni nini ?
Hali kama hii ikiruhusiwa kuendelea, katika siku zijazo watu wasiopenda muungano wa klabu hii wataendelea kupinga mtu asiyetokea Magharibi mwa nchi kuongoza klabu hii.
Ni ukweli usiopingika kuwa mashabiki wengi wa AFC Leopards wanatokea eneo la Magharibi, lakini kuna mashabiki wa klabu hiyo kutoka Pwani, eneo la Kati na hata nje ya nchi.Hii ni klabu ya watu wote.
Wakati Alex Ole Magelo alipokuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo miaka kadhaa iliyopita hapakuwa na siasa kama hizi lakini aliendelea kupigwa vita kwa sababu yeye sio wa jamii inayoaminiwa kumiliki klabu hiyo.
Ni vema kufahamu kuwa AFC Leopards haipo tena kikabila, tumeshuhudia makocha mbalimbali wakiwasajili wachezaji kutoka maeneo mengine ya nchi akina Otieno, Mutisya, Mwangi, Mwachoni sasa wanaichezea klabu hii.Huu ndio mwelekeo kamili.
Tumewaona pia viongozi kutoka maeneo mengine ya nchi wakijitokeza kufadhili klabu hiyo mfano ni aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Katika mazingira haya, hakuna mfadhili anayeweza kuvumilia siasa kama hizi zenye mrengo wa kikanda.
Tofauti kama hizi pia zinaweza kusababisha vurugu miongoni mwa wachezaji na hata viongozi.
Msimu uliopita, vurugu katika klabu ya Gor Mahia watani wa jadi wa Leopards zilisababiha mfadhili wao wakati huo kampuni ya maziwa Brookside kujiondoa. Hii inaweza wazi kuwa hakuna aneyetaka vurugu au siasa chafu katika mchezo wa soka.
Sababu nyingine inayoweza kumkimbiza mfadhili ni matumizi mbaya ya fedha. Ukiwa mwizi, ikiwa wewe si mwaminifu hakuna anayeweza kukuamini kamwe. Je, pamoja na suala la ukabila katika kalbu hii, viongozi wamejiuliza ikiwa ni waaminifu kwa wafadhili ?
Ikiwa mawazo haya potofu yataendelea kuitawala klabu hii, basi itakuwa ni vigumu kwa viongozi kudumu na wafadhili hawatakuwa tayari kutoa fedha zao kwa Ingwe.
Wachezaji wanatia huruma sana unapowasikia wakilalamika kuwa hawajalipwa kwa miezi kadhaa, hali ambayo inawakosesha raha na hata kiwango cha uchezaji wao kinarudi nyumbani.
Katika mazingira kama haya klabu hii inaweza kumpoteza kocha Zdravko Logarusic raia wa Croatia ambaye ameonekana kuinua kiwango cha klabu hiyo katika siku za hivi karibuni.
Licha ya changamoto hizi, AFC Leopards ina nafasi ya kujikwamua katika mazingira haya ikiwa wadau wa klabu hii watabadilisha mawazo yao na kuacha mawazo ya kizamani kuwa klabu hii ni ya Waluhya.
Wafadhili wapo tayari kuifadhili klabu hii kubwa, lakini wanachungulia kujihakikishia kuwa nyumba ya AFC ni safi. Wafhadili hawapendi siasa za chuki na za kuwagawa watu.Wadau wa klabu hii wasitumie nyadhifa zao kuimarika kisiasa.
Hii ni changamoto kwa mashabiki na viongozi wa AFC Leopard alimaarufu kama Ingwe.
Haya yakikosolewa mambo yanaweza yakawa mazuri.