Na Victor Abuso,
Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limezindua jezi mpya za timu za Taifa, zitakazokuwa zikitumika katika michuano mbali mbali ya kimataifa.
TFF imezindua jezi tatu, ambazo ni jezi za ugenini, jezi za nyumbani na jezi zitakazokuwa zikitumika kwa ajili ya mazoezi.
Jezi hizo zenye bendera ya nchi za rangi ya samawati (Bluu), nyeupe na pamoja na nyingine ya samawati na mstari mweupe.
Jezi hii imezinduliwa wakati huu Taifa Stars ikijiandaa kushiriki katika michuano ya kufuzu katika fainali za mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.
Kikosi cha Tanzania kimeondoka siku ya Alhamisi kwenda nchini Ethiopia kwa maandalizi ya mchuano wake wa kwanza wa kutafuta tiketi ya AFCON dhidi ya Misri tarehe 14 mwezi huu.
Mbali na Misri, Tanzania imeorodheshwa katika kundi moja na Nigeria na Chad.
Kocha Mart Nooij aliyepewa kazi ya kuhakikisha Stars inafuzu fainali za CHAN au ajiuzulu, amesema kikosi chake kipo tayari kupambana katika michuano hii.
Kikosi cha Taifa Stars :
Mohamed Hussein, Peter Manyika, Hassan Isihaka, Jonas Mkude (Simba), Salum Telela, Juma Abdul, Nadir Haroub (Yanga), Aishi Manula, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Kelvin Friday (Azam FC), Rashid Mandawa, Atupele Green (Kagera Sugar), Haroun Chanongo (Stand United) Malimi Busungu (Mgambo JKT) na Emmanuel Simwanda (African Lyon). Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe , DR Congo.)