Connect with us

Na Paul Manjale,Dar Es Salaam,

YANGA SC sasa inahitaji kushinda mchezo mmoja tu kati ya miwili iliyosalia ili iweze kuweka rekodi safi ya kutwaa mara tatu mfululizo ubingwa wa ligi kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya jioni ya leo kuifunga timu ngumu ya Mbeya City ya mkoani mabao 2-1 katika mchezo mkali ulioisha hivi punde kwenye Uwanja wa Taifa,Dar Es Salaam.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na Mwamuzi Andrew Shamba wa Pwani,ilishuhudia dakika 45 za kipindi cha kwanza zikimalizika Yanga SC wakiwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa kwa kichwa na winga wake Simon Msuva ambaye alikuwa akifunga bao lake la 14 msimu huu.

Msuva alifunga bao hilo katika dakika ya 7 akiunganisha krosi safi ya Hassany Kessy Ramadhani kutoka wingi ya kulia.Hata hivyo Msuva hakuweza kuendelea na mchezo mara baada ya kufunga bao hilo kwani aligongana na beki mmoja wa Mbeya City na kupata mpasuko juu ya jicho.

Kipindi cha pili Mbeya City walikianza kwa nguvu na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 58 kupitia kwa Haruna Shamte.Shamte alifunga bao hilo kwa shuti la karibu baada ya mabeki wa Yanga SC wakiongozwa na Nahodha Nadir Haroub ‘Canavarro’ kushindwa kuondoa hatari langoni mwao.

Mzambi Obrey Chirwa aliisafishia Yanga SC njia ya kutetea ubingwa wake iliyoutwaa katika misimu miwili iliyopita baada ya kuifungia bao la pili katika dakika ya 64 kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Juma Abdul.

Ushindi huo umeifanya Yanga SC irejee kileleni mwa msimamo wa ligi kuu baada ya kufikisha pointi 65 katika michezo 28.Wapinzani wao Simba SC wameshuka mpaka nafasi ya pili ikiwa na pointi zake 65 katika michezo 29.Yanga SC iko kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga.

Katika michezo mingine ya leo Kagera Sugar imeichapa Mbao FC mabao 2-1.Tanzania Prisons imeifunga Ndanda FC mabao 2-1.Majimaji FC wakiwa ugenini Mkwakwani,Tanga wameishusha daraja JKT Ruvu baada ya kuifunga bao 1-0.Mtibwa Sugar wameifunga Mwadui FC mabao 4-2.

African Football Writer contributing @Soka25east | Commentator; appeared on @MySoccerAfrica, @KweseSports, @ntvkenya, others | Keen follower of African Football. E-mail: bonfaceosano@gmail.com

More in