Na Victor Abuso,
Makamu wa rais wa pili wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF Almany Kabele, amezuru jijini Kigali nchini Rwana na kusema amefurahishwa na maandalizi ya nchi hiyo kuwa wenyeji wa michuano ya mataifa ya Afria baina ya wachezaji wanaocheza soka nyumbani CHAN mapema mwakani.
Michuano hiyo ya CHAN itaanza kuchezwa tarehe 16 hadi tarehe 7 mwezi wa Februari mwaka 2016 katika jiji la Kigali, mjini Huye na Rubavu.
Siku ya Jumanne Kabele ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati andalizi ya michuano hiyo baada ya kuzuru uwanja wa Kimataifa wa Amahoro pia Stade Umuganda na Huye na alidokeza kuwa anaridhishwa na kazi inayoendelea katika viwanja hivyo.
Rais wa Ferwafa Vincent Nzamwita amesema, “ Kabale ametemebelea viwanja vyote vitakavyotumiwa na amekubaliana nasi kuwa maandalizi yanakwenda vizuri kabisa,”.
Nzamwita ameongeza kuwa Makandarasi wamemwahidi kuwa kufikia mwezi Septemba mwaka huu, viwanja vyote vitakuwa tayari kwa michuano hiyo na hivyo hakuna kitakachoizua Rwanda kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya CHAN.
CAF itatuma tena wakaguzi wake mwezi Septemba kuona maandalizi yatakapokuwa yamefikia kabla ya droo ya mataifa yatakayoshiriki kufanyika mwezi Novemba.
Michuano ya kufuzu kushiriki katika michuano hii itafanyika kuanzia tarehe 19 mwezi Juni hadi mwisho wa mwezi Agosti ili kupata mataifa 15 yatakayoshiriki katika michuano hiyo.
Amavubi Stars ya Rwanda wao wameshafuzu kwa sababu ni wenyeji na wamepangiwa mchuano wa Kimataifa wa kirafiki tarehe 25 mwezi ujao dhidi ya Afrika Kusini jijini Johannesburg.
Makala ya kwanza ya michuano ya CHAN yalifanyika mwaka 2009 nchini Cote Dvoire na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC) ilikuwa nchi ya kwanza kushinda taji hilo.
Michuano ya mwisho ilifanyika mwaka 2014 nchini Afrika Kusini na Libya wakaibuka mabingwa.