Connect with us

Timu za taifa za michezo wa soka za Burundi, DRC na Uganda, kutoka eneo la Afrika Mashariki na Kati, zilianza vizuri kampeni ya kufuzu kucheza fainali ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon baada ya kuandikisha ushindi mwishoni mwa wiki iliyopita.

 Wakicheza jijini Bujumbura katika uwanja wa Prince Louis Rwagasore, Burundi iliifunga Sudan Kusini mabao 3-0.

Intamba Murugamba ilipata mabao yote katika kipindi cha kwanza cha mchuano huo huku wachezaji Amissi Tambwe, Gael Duhayindavyi na Abdul Razak wakiipa ushindi timu yao.

Burundi inaongoza kundi la C kwa alama tatu sawa na  Mali. Mchuano ujao utakuwa ni mwezi Machi mwaka 2018 dhidi ya Gabon.

Nayo Leopard ya Jamhuri ya Kidemokrasia ikicheza nyumbani jijini Kinshasa, iliifunga jirani yake Congo Brazaville mabao 3-0.

Cedric Bakambu aliifungia timu yake mabao mawili, huku Chancel Mbemba akifunga bao la tatu katika dakika 90 ya mchuano huo.

Leopard imejumuishwa katika kundi moja na Zimbabwe na Liberia.

Geoffrey Sserunkuma aliipa Uganda ushindi katika dakika ya 83 ya mchuano wake dhidi ya Cape Verde jijini Praia.

Ushindi huu umeifanya Uganda kuongoza kundi la L kwa alama 3, huku ikifuatwa na Lesotho na Tanzania ambao wana alama moja.

Hata hivyo, mataifa mengine ya Afrika Mashariki yalianza vibaya katika michuano hii baada ya kutoka  sare au kufungwa katika mechi zao za kwanza.

Matokeo mengine:-

  • Tanzania 1-1 Lesotho
  • Kenya 1-2 Sierra Leone
  • Jamhuri ya Afrika ya Kati 2-1 Rwanda
  • Ghana 5-0 Ethiopia

More in East Africa