Na Victor Abuso,
Rais wa Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF, Jamal Malinzi amesisitiza kuwa kocha wa timu ya taifa Mart Nooij hataachishwa kazi baada ya Misri kuishinda Taifa Stars mabao 3 kwa 0 katika mchuano wa kwanza kufuzu katika fainali za michuano ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.
Rais huyo wa TFF ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam kutuliza shinikizo kutoka kwa wapenzi wa soka nchini humo wanamtaka kocha huyo kufutwa mara moja kutokana na matokeo mabaya.
Malinzi ameongeza kuwa wao kama viongozi wa soka hawawezi kukurupuka na uamuzi wa kumfuta kazi kocha Nooij na kwenda kinyume na makubaliano ya Kamati kuu ya soka nchini humo.
Mwezi uliopita, Kamati kuu ya TFF ilifikia uamuzi kuwa kocha Nooij atafutwa kazi iwapo Uganda itawaondoa katika michuano ya mzunguko wa kwanza ya kutafuta tiketi ya kufuzu katika michuano ya CHAN baina ya wachezaji wanaocheza soka nyumbani.
“Siwezi kwenda kinyume na uamuzi wa Kamati kuu, na tutasubiri kuona mwenendo wa timu ya taifa katika michuano hii ya CHAN,” alisisitiza Malinzi.
Tanzania inajiandaa kumenyana na Uganda katika mchuano wa kwanza wa kufuzu katika michuano hiyo ya CHAN itakayochezwa mwishoni mwa juma hili visiwani Zanzibar, kabla ya kurudiana baada ya majuma mawili jijini Kampala mapema mwezi ujao.
Kocha Nooij alipewa nafasi mwisho kuiongoza Stars kufuzu michuano ya CHAN baada ya kufanya vibaya katika michuano ya kuwani ubingwa wa mataifa ya Kusini mwa Afrika COSAFA.
Rwanda itakuwa mwenyeji wa michuano hii mapema mwaka ujao.