Na Victor Abuso,
Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF, limetangaza kumfuta kazi kocha wa timu ya taifa Mholanzi Mart Nooij baada ya matokeo mabaya katika michuano ya Kimataifa.
Hatua hii inakuja baada ya Tanzania kufungwa mabao 3 kwa 0 na Uganda katika mchuano wa kwanza kufuzu katika michuano ya CHAN baina ya wachezaji wanaocheza soka nyumbani.
Mchuano huo wa Jumamosi ulifanyika katika uwanja wa Amman visiwani Zanzibar matokeo ambayo yamewakera wadau wa soka nchini humo kabla ya mchuano wa marudiano mwanzoni mwa mwezi ujao jijini Kampala.
Rais wa TFF, katika ujumbe wake katika ukurasa wa twitter alisema kuwa wameamua kuachana na kocha Nooij na uongozi wa kiufundi wa taifa Stars.
Baada ya mchuano huo wa Jumamosi usiku, Malinzi aliandika haya, “Kamati ya utendaji ya TFF imesitisha ajira ya kocha mkuu wa timu ya Taifa Maart Nooij pamoja na benchi lake zima la ufundi kuanzia kesho,”.
TFF ilikuwa imempa Nooij kibarua cha kufuzu katika michuano ya CHAN la sivyo aachishwe kazi na kwa matokeo ya mchuano wa nyumbani imeonekana kuwa hataweza kuisaidia Taifa Stars kwenda Rwanda mwakani.
Mrisho Ngasa mchezaji wa kulipwa katika klabu ya Free State Stars nchini Afrika Kusini amesema shinikizo kutoka kwa mashabiki zimesababisha taifa Stars kupata matokeo mabaya.
Katika ukurasa wake wa Twitter aliandika, “Presha ya mashabiki, ni kubwa Sana, panic kwa wachezaji inaongezeka, si rahisi kupata matokeo chanya,”.
Masaibu ya Taifa Stars yameendelea kushuhudiwa katika msururu wa michuano ya Kimataifa juma moja tu baada ya kufungwa na Misri mabao 3 kwa 0 katika mchuano wa kufuzu katika fainali ya michuano ya bara Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.