Uchaguzi wa kamati ya uongozi ya ligi ya Tanzania bars utafanyika tarehe 15 Oktoba mwaka huu.
Taarifa kutoka kwa shirikisho LA Mpira wa miguu Tanzania imesema
UCHAGUZI KAMATI YA UONGOZI TPLB
Uchaguzi wa Kamati ya Uongozi (Management Committee) ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara utafanyika Jumapili Oktoba 15, 2017 jijini Dar es Salaam.
Fomu kwa ajili ya wagombea zitaanza kutolewa Agosti 17, 2017 kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu kwa wagombea ni saa 10.00 jioni Agosti 23, mwaka huu.
Nafasi zitakazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watatu kuwakilisha klabu za Ligi (PL), Wajumbe wawili wa kuwakilisha klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na Mjumbe mmoja wa kuwakilisha klabu za Ligi Daraja la Pili (SDL).
Ada ya fomu kwa nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ni Sh 200,000 (Shilingi lakini mbili) wakati nafasi nyingine zilizobaki ni Sh 100,000 (Shilingi laki moja).
Uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013.
Wagombea kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa Bodi ya Ligi Kuu ni marais au wenyeviti wa klabu husika.
Wagombea wanatakiwa kuwa wenyeviti au Marais wa klabu husika.
Nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inagombewa na klabu za Ligi Kuu pekee.
MALALAMIKO YA KLABU KATIKA USAJILI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea malalamiko kutoka baadhi ya timu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji vya soka zikidai fidia baada ya wachezaji wao kusajiliwa na klabu nyingine msimu wa 2017/18.
Jana Agosti 14, 2017 ilikuwa siku ya mwisho kwa timu na vituo vya kuibua na kukuza vipaji kuwasilisha malalamiko yao TFF kuhusu fidia za mafunzo; ada ya usajili; ada za maendeleo na kuvunjwa kwa mikataba kutoka katika timu walizochezea hadi msimu uliopita.
TFF imepokea malalamiko ya Kagera Sugar ya Kagera dhidi ya Azam FC ya Dar es Salaam kuhusu mchezaji Mbaraka Yussuf wakati Majimaji ya Songea pia imelalamika Azam kuhusu mchezaji Idd Kipangwile.
Alliance ya Mwanza imelalamikia Pamba pia ya Mwanza kuhusu mchezaji Juma Nyangi ambako madai hayo yamekwenda mbali zaidi yakisema kuwa mchezaji husika amebadili jina kwa lengo la kudanganya.
Kwa upande wake, African Lyon imeondokewa na wachezaji 19 na inadai fidia katika timu, wachezaji kwenye mabano za Majimaji (Saleh Malande); Lipuli (Hamad Manzi, Lambele Reuben na Mussa Nampoka); Young Africans (Rostand Youthe Jehu); Tusker FC (Abdul Hilal) na Ndanda kwa wachezaji Hamad Tajiri na Baraka Majogoo.
Madai mengine ni dhidi ya Coastal Union kwa wachezaji Baraka Jaffary, Omary Salum, Raizen Hafidh na Fred Lewis huku madai mengine ni kwa Kagera Sugar kwa wachezaji Omar Abdallah, Abdallah Mguhi na Vicent Ludovic na Alhaji Zege .
Madai mengine ni dhidi ya timu ya Kinondoni Municipality Council (KMC) ambayo imewasajili Halfan Twenye, Yussuf Abdul na Rehani Kibingu wakati Singida United inalalamikiwa kumsajili Miraji Adam ilihali Njombe Mji inadaiwa fidia kwa kumsajili mchezaji Salum Juma.
Malalamiko mengine ni ya Kisa Academy ya Kinondoni, Dar es Salaam dhidi ya timu za Mbeya City (Idd Seleman); Majimaji (Jafar Mohammed); Mbao (Ally Rashid); Stand United (Said Mbati) na Friends Rangers (Hassan Abubakar).
Madai mengine dhidi ya timu za Coastal Union (Abubakar Nyakarungi na Ahmed George); The Mighty Elephant (Maliki Hamad); Kagera Sugar (Hussein Idd) na Azam FC (Omary Maunda).
Kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kinatarajiwa kuketi Jumapili kupitisha usajili lakini kabla kitapitia malalamiko hayo na kuchukua uamuzi.
MAANDALIZI MECHI YA NGAO YA HISANI
Maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii utakaowakutanisha Mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2016/17, Young Africans na Mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup), Simba yanakwenda vema.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linapenda kuwatangazia umma kuwa viingilio katika mchezo huo vimepangwa katika makundi manne.
Sehemu ya VIP ‘A’ tiketi zake ni Sh 25,000; sehemu ya VIP ‘B’ na ‘C’ Sh 20,000; Viti vya Rangi la Chungwa Sh 10,000 na mzunguko kwa vitu vya rangi za bluu na kijani ni Sh 7,000.
Tiketi zimeanza kuuzwa leo Jumanne Agosti 15, 2017 ili kuwapa fursa wadau wa mpira wa miguu kununua tiketi mapema kujipeusha na usumbufu.
KIKAO KLABU ZA LIGI DARAJA KWANZA
Viongozi wa Klabu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL), wanatarajiwa kuwa na kikao na uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB), kitakachofanyika Ijumaa Agosti 8, 2017 kuanzia saa 3.00 asubuhi kwenye Hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kitakuwa maalumu kwa ajili ya kujadili Ligi Daraja la Kwanza lakini pia kutoa semina kwa viongozi hao kuhusu Leseni za Klabu (Club License).
TFF inatoa wito kwa viongozi wa juu wa klabu kuhudhuria kikao hicho muhimu . TFF ingependa kusisitiza kuzingatia muda wa kuanza kikao.
……………………………………………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
talking African football