Na Victor Abuso.
Klabu ya Azam FC kutoka Tanzania imeshinda taji la soka Afrika Mashariki na Kati CECAFA baina ya vlabu baada ya kuishinda Gor Mahia ya Kenya mabao 2 kwa 0 katika fainali ya kufana iliyochezwa jioni hii katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam nchini Tanzania.
Azam FC imeshinda taji hili kwa mara ya kwanza na hadi kunyakua taji hili haikufungwa bao hata moja katika muda wa dakika tisini.
Mabao ya Azam yalitiwa kimyani na nahodha John Bocco dakika ya kumi na sita kipindi cha kwanza baada ya kupata pasi murua kutoka kwa mshambuliaji Kipre Cheche ambaye pia alifunga bao la pili na la ushindi katika dakika ya 64 .
Beki ya Azam ikiongozwa na Pascal Wawa raia wa Cote Divoire iliisumbua sana Gor Mahia mbele ya mamia ya mashabiki wake waliosafiri kutoka jijini Nairobi kuishabikia timu yake.
Mshambuliaji wa Gor Mahia Michael Olunga aliibuka mfungaji bora kwa kuifungia timu yake mabao matano.
Mara ya mwisho Gor Mahia kushinda taji hili ili kuwa ni miaka 30 iliyopita wakati michuano hii ilifanyika nchini Sudan.
Azam pamoja na taji, imepata Dola za Marekani Elfu 30, Gor Mahia Dola Elfu 20 na KCCA ya Uganda iliyomalizika katika nafasi ya tatu ikipata Dola Elfu 10.
Katika Historia ya michuano hii Azam wameshinda mara moja na Gor Mahia mara tano.