Na:Victor Abuso
Klabu ya soka ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaendelea kuongoza kundi la A katika michuano ya makundi kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika.
Mwishoni mwa juma hili, Mazembe ikiwa nyumbani katika uwanja wake mjini Lubumbashi iliifunga Smouha ya Misri bao 1 kwa 0 na sasa inaongoza kundi lao kwa alama nane.
Huu ni ushindi wa pili dhidi ya klabu hii ya Misri kwa sababu mchuano wa kwanza mjini Alexandria mwezi uliopita, TP Mazembe walipata ushindi wa mabao 2 kwa 0 wakiwa ugenini.
Mchuano mwingine wa TP Mazembe ni tarehe 23 mwezi huu dhidi ya Al-Hilal ya Sudan na katika mchuano wa kwanza walitoka sare ya kutofungana.
Al Hilal na Mogreb Tetoun ya Morroco wana alama tano katika kundi hili huku Smouha ikiwa ya mwisho kwa alama tatu.
Katika kundi B, Al Merrikh ya Sudan inapambana na Es Setif ya Algeria na siku ya Jumsmosi, USM Alger pia ya Algeria waliwashinda ndugu zao MC El Eulma pia ya Algeria bao 1 kwa 0.
Kundi hilo linaongozwa na USM Alger ambao wana alama 12 na wamefuzu katika hatua ya nusu fainali, nafasi ya pili ni ya Al-Merrikh ambao ina alama 4 sawa na Es Setif ya Algeria.