Na Victor Abuso
Kamati ya rufaa ya Shirikisho la soka nchini Uganda, imeirejesha klabu ya Lweza FC katika ligi ya soka nchini humo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Richard Kiboneka amesema kuwa klabu ya Lweza FC imetimiza masharti muhimu yaliyokuwa yanahitajika ili kuendelea kusalia katika ligi hiyo.
Taarifa hizi zimepokelewa kwa furaha kubwa na viongozi na mashabiki wa klabu hiyo yenye makao yake katika mtaa wa Kajjansi jijini Kampla.
Msemaji wa klabu hiyo Abdul Suleiman Semugenyi ameiambia soka25east.comkuwa baada ya kushinda rufaa hiyo kazi iliyo mbele yao ni kuendelea kuimarisha klabu hiyo na kuwasajili mashabiki zaidi.
“Nina furaha kubwa sana baada ya klabu yetu kushinda rufaa hii, walidai kuwa hatuna uwanja, Ofisi na makocha wetu hawana leseni ya CAF na hilo limedhirika kuwa sio kweli,” alisema Semugenyi.
Uongozi wa Lweza FC awali ulidai kuwa uamuzi wa kuwashusha daraja ulichukuliwa bila ya kuwashirikisha na madai yaliyoorodheshwa hakuwa sahihi.
Lweza FC sasa imepangiwa kumeyana na BUL FC katika mchuano wake wa ufunguzi wa msimu mpya wa mwaka 2015/16 siku ya Jumamosi.
Orodha kamili ya michuano ya ufunguzi wa ligi mwishoni mwa wiki:-
Vipers Vs Saints – Uwanja wa Buikwe
Sadolin Vs KCC – Uwanja wa Bugembe
Express Vs Police – Uwanja wa Mutesa II, Wankulukuku
Soana Vs Bright Stars – Uwanja wa Kavumba