Connect with us

 

Burkina Faso itachuana na Misri katika hatua ya nusu fainali kuwania taji la bara Afrika AFCON inayoendelea nchini Gabon.

Mchuano huu utachezwa siku ya Jumatano katika uwanja wa Amitie jijini Libreville.

Burkina Faso ilifuzu katika hatua hii baada ya kuishinda Tunisia mabao 2-0 mwishoni mwa wiki iliyopita katika uwanja wa Port-Gentil.

Aristide Bance na Prejuce Nakoulma ndio walioifungia Burkina Faso mabao muhimu katika dakika ya 80 na 85 ya mchuano huo.

Ikiwa Burkina Faso itashinda mechi ya nusu fainali, itafuzu katika hatua ya fainali kama ilivyokuwa mwaka 2013 nchini Afrika Kusini.

Misri nayo inalenga kufika katika fainali, baada ya kufanya hivyo mwaka 2010 waliponyakua taji hili mara ya mwisho. Misri inaendelea kushikilia rekodi ya michuano hii kwa kushinda mara saba.

Nusu fainali nyingine itakuwa ni kati ya Cameroon na Ghana siku ya Alhamisi.

Cameroon ambayo ilishinda taji hili mara ya mwisho 2002 itamenyana na Ghana ambayo mara ya mwisho kushinda taji hili mara mwaka 1982.

Ghana itasaka kufika hatua ya fainali baada ya kufanya hivyo mwaka 2015 nchini Equitorial Guinea lakini ikafungwa na Ivory Coast kupitia mikwaju ya Penalti.

Black Stars ilifuzu mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kuifunga Leopard ya DRC kwa mabao 2-1 katika uwanja wa Oyem.

Ghana ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 63 ya mchuano huo kupitia Jordan Ayew lakini DRC ilisawazisha kupitia Paul-Jose M’poku katika dakika 68.

Hata hivyo, mambo yalikuwa mbaya zaidi kwa DRC baada ya Ghana kupata penalti katika dakika ya 78 na Andrew Ayew kutikisa nyavu.

Wachambuzi wa soka wanasema kuwa mchuano kati ya Ghana na Cameroon unatarajiwa kuwa mgumu sana na labda kuonekana na wengi kama fainali ya michuano hii.

Misri nao walikatisha matumaini ya Morocco baada ya kupata ushindi wa bao 1-0.

Bao pekee ya Misri lilitiwa kimyani na Mahmoud Kahraba katika dakika ya 88 ya mchuano huo na kudidimiza matumaini ya kocha wa Morroco Herve Renard kusaka ubingwa wa taji hili mara tatu na mataifa tofauti.

Mwaka 2012, aliisaidia Zambia kushinda taji hili, lakini mwaka 2015 aliingoza Ivory Coast kunyakua ushindi.

Fainali ya michuano hii itachezwa siku ya Jumapili katika uwanja wa Stade de L’Amitie jijini Libreville.

More in