Timu ya taifa ya Tanzania, taifa Stars, hii leo imeshindwa kuwika mbele ya mafarao wa Misri baada ya kukubali kufungwa mabao 2-0 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Timu ya taifa ya Misri ilikuwa inahitaji ushindi kwenye mchezo wa leo ili kujihakikishia kupata tiketi yake ya kushiriki michuano ya Afrika itakayofanyika nchini Gabon.
Tanzania ilikuwa inahitaji ushindi wa mabao angalau 3-0 dhidi ya Misri ili ijihakikishie nafasi ya kufuzu kwakuwa kama ingepata ushindi Dar es Salaam, ingehitaji pia kupata ushindi dhidi ya timu ya taifa ya Nigeria “The Super Eagles”.
Kwa matokeo haya sasa, yanamaanisha kuwa timu ya taifa ya Misri inakata rasmi tiketi ya kucheza fainali za kombe la mataifa ya Afrika nchini Gabon, kwakuwa wanamaliza mechi zake ikiwa na alama 10 kibindoni.
Tanzania itaenda kumaliza ratiba yake kwa kucheza na Nigeria mwezi mmoja ujao, ambapo kwenye msimamo Nigeria ina alama mbili ikiwa katika nafasi ya pili, huku Tanzania ni ya tatu ikiwa na alama 1 na Chad ni ya mwisho ikiwa haina alama baada ya kujitoa kwenye mashindano haya.