Burkina Faso na Misri zinamenyana katika mchuano muhimu wa nusu fainali kutafuta taji la 31 ya michuano ya soka baina ya Mataifa ya Afrika AFCON, inayoendelea nchini Gabon.
Mataifa haya mawili yanakwenda katika michuano hii baada ya kupata ushindi katika mechi zao zote.
Mchuano huu unachezwa katika uwanja wa Kimataifa wa Amitie jijini Libreville.
Mwamuzi wa kati wa mchuano wa leo ni Malang Diedhiou kutoka Senegal.
Misri inashikilia rekodi ya kushinda taji hili mara saba, mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 2010. Imewahi kushinda pia taji hili mwaka 1957,1959, 1986, 1998, 2006 na 2008.
Burkina Faso nayo ina rekodi ya kufika katika hatua ya fainali mwaka 2013 dhidi ya Nigeria, lakini kwa bahati ikashindwa kunyakua taji.
Mapharaoh walifanikiwa kuwaondoa Morocco katika hatua hii ya nusu fainali mwaka 1986, lakini pia Burkina Faso mwaka 1998.
Mwaka 2006, iliishinda Senegal, mwaka 2008 Ivory Coast na Algeria mwaka 2010 ili kufika fainali.
Mshindi wa mchuano huu atachuana na Cameroon au Ghana katika hatua ya fainali mwishoni mwa wiki hii.
Cameroon na Ghana zitachuana katika hatua ya nusu fainali ya pili siku ya Alhamisi.