Na: Victor Abuso
Timu za taifa za soka kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati mwishoni mwa juma hili zinashuka dimbani katika viwanja mbalimbali barani Afrika, kuanza michuano ya kufuzu katika fainali za kutafuta ubingwa wa Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.
Jumapili hii, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itakuwa katika uwanja wa Tata Raphael jijini Kinshasa kumenyana na Madagascar.
Kocha Florent Ibengé ambaye aliisaidia timu yake katika michuano iliyopita iliyofanyika mwaka huu nchini Equitorial Guinea.
Wachezaji wanaotegemewa ni pamoja na Issama Mpeko , Mubele Ndombe, Jean Kasusula na Dieumerci Mbokani.
Licha ya machafuko yanayoendelea katika nchi yao, Sudan Kusini itakuwa ugenini kumenyana na Mali.
Sudan Kusini imejumuishwa katika kundi moja na Benin na Equitorial Guinea.
Uganda Cranes ambayo ilifuzu mara ya mwisho katika michuano ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka 1978, itakuwa nyumbani katika uwanja wa Naambole kumenyana na Boswana.
Mataifa megine katika kundi hili ni Comoros na Burkina Faso.
Uganda imekaribia kufuzu katika michuao hii mara mbili lakini kutokana na kutofanya vizuri katika michuano ya ugenini imewakosesha kufuzu tena katika michuano hiyo.
Vijana wa kocha Micho Sredojevic wana rekodi nzuri nyumbani katika michuano minane waliocheza nyumbani wameshinda saba, rekodi ambayo mashabiki wa Cranes wanatumai kuwa wataendeleza siku ya Jumamosi.
Harambee Stars ya Kenya ipo katika kundi moja na Zambia, Congo Brazaville na Guinea Bissau.
Kenya inayofunzwa na Bobby Williamson inaanza mapambano ya kufuzu katika fainali hizi dhidi ya Congo Brazaville ugenini.
Mara ya mwisho kwa Kenya kufuzu katika michuano hii ilikuwa ni mwaka 2004 wakati michuano hii ilipoandaliwa nchini Tunisia.
Rwanda ambayo pia ilifuzu mara ya kwanza mwaka 2004, itaanza kampeni yake dhidi ya Msumbubiji mjini Maputo.
Mbali na Msumbiji, Rwanda imepangwa katika kundi moja na Mauritius na Ghana.
Sudan itamenyana na Sierre Leone jijini Khartoum, katika kundi ambalo pia lina mwenyeji wa michuano hiyo ya Afrika mwaka 2017 Gabon.
Intamba Murugamba ya Burundi nao watakuwa jijini Dakar nchini Senegal kumenyana na Teranga Lions katika mchuano wake wa kwanza katika kundi ambalo pia lina Niger na Namibia.
Taifa Stars ya Tanzania itakuwa na kazi nchini Misri katika uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.
Mbali na Tanzania, taifa Stars imepangwa pia na Nigeria na Chad.
Uongozi wa soka nchini Tanzania umempa kocha Mholanzi Mart Nooij nafasi nyingine ya kudhihirisha kuwa kikosi chake kinaweza kufuzu katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika baada ya matokeo mabaya katika michuano ya mwezi uliopita wa Kusini mwa Afrika COSAFA.