Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya soka ya Nigeria Stephen Keshi, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 54.
Kifo cha Keshi ambaye aliingia katika vitabu vya historia kwa kuwa kocha na mchezaji wa zamani kuiongoza nchi yake kunyakua taji la ubingwa wa Afrika mwaka 2013, kilithibitishwa na Shirikisho la soka nchini humo NFF.
Vyombo vya Habari nchini Nigeria vinaripoti kuwa kifo cha Keshi kilishababishwa na mshtuko wa moyo.
Keshi pia aliwahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Togo na Mali lakini aliwahi pia kucheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji katika klabu ya Anderlecht.
Mwaka 2014, aliingoza Nigeria hadi katika hatua ya 16 wakati wa michuano ya kombe la dunia nchini Brazil.
Baada ya michuano ya kombe la dunia, alifutwa kazi lakini rais wa wakati huo Goodluck Jonathan aliamuru arejeshwe kazini.
Alifutwa kazi rasmi mwaka mwaka uliopita mwezi Julai.
Kifo cha kocha huyu kumeleta huzuni kubwa kwa wapenzi wa soka nchini Nigeria na barani Afrika.
Rais wa Shirikisho la soka nchini Tanzania, TFF Jamal Malinzi katika ukurasa wake wa Twitter amesema, “TFF inaugana na Shirikisho la soka nchini Nigeria NFF, kuomboleza kifo cha Keshi,”.
Kocha wa timu ya taifa ya Uganda Milutin Micho naye katika ukurasa wale wa Twitter amesema, “ Nguli wa soka barani Afrika “The Big Boss” Keshi ametuacha mapema sana. Soka nchini Nigeria na bara Afrika halitasahau kazi nzuri uliyofanya Togo,Mali na Nigeria,”.
Kifo hiki kimekuja baada ya kufariki dunia kwa mkewe Kate baada ya kuugua saratani kwa miaka mitatu.