Baada ya kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF, Ahmad Ahmad anasubiriwa kuleta mabadiliko ambayo yanalenga kubadilisha usimamizi wa soka barani Afrika.
Wakati wa kampeni, Ahmad aliahidi kuleta usimamizi upya katika Shirikisho hilo, utakaowafanya wadau wote wa soka kujihisi kuhusika moja kwa moja na uongozi wa CAF.
Akizungumza na Shirika la Habari la Uingereza la BBC, rais mpya wa CAF amesema kazi yake ya kwanza ni kuthathmini hali ya kifedha katika Shirikisho hilo.
Raia huyo wa Madagascar ameongeza kuwa baada ya kwenda Cairo, ambako ndio makao makuu ya CAF, atakwenda kuangalia namna fedha zimekuwa zikitumika na namna viongozi waliopita walikuwa wanafanya kazi zao kabla ya kusonga mbele na kuanza kutekeleza maono yake.
Mchezaji huyo wa zamani lakini pia kocha anatarajiwa kuongoza CAF kwa miaka minne ijayo hadi mwaka 2021.
Mbali na kuwa rais mpya wa CAF na rais wa Shirikisho la soka nchini mwake, ni Seneta katika taifa lake.
Ahmad Ahmad alimshinda Issah Hayatou kwa kupata kura 34.
Hayatou ambaye ameongoza CAF kwa muda wa miaka 29 alipata kura 20.