Klabu ya Al Masry ya Misri imewasili nchini Tanzania kwa mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya timu ya Simba SC ya Tanzania utakaochezwa Jumatano ijayo katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Al Masry inayonolewa na Kocha Hossam Hassan imewasili nchini Tanzania ikiwa na wachezaji 21 akiwemo mshambuliaji hatari kutoka Burkinafaso Aristide Bance.
Al Masry imewasili alfajiri ya leo kwa ajili ya mchezo huo unasubiriwa kwa hamu na ghamu na mashabiki wa soka nchini Tanzania na utaanza saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Simba ilifuzu hatua ya awali kwa kuiondoa Gendermarie ya Djibout kwa mabao 5-0 wakati wapinzani wao Al Masrywalifuzu hatua hiyo kwa kuishinda Green Buffalo ya Zambia kwa mabao 5-2.
Tayari klabu ya Simba kupitia Ofisa wa Habari, Haji Manara imesema kikosi chake kimeongezewa nguvu na urejeo wa wachezaji Emanuel Okwi na John Bocco waliokuwa na majeraha. Wachezaji hao walikosa mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Stand United ambao Simba ililazimishwa sare ya mabao 3-3.
Wakati huohuo, Yanga itashuka uwanjani keshokutwa Jumanne kucheza na timu ya Township Rollers ya Botswana katika mchezo wa klabu bingwa barani Afrika.
Yanga ilifuzu hatua mzunguko wa kwanza kwa kuindoa Saint Louis ya Shelisheli wakati Rollers iliwaondoa miamba ya Sudan, Al Merreikh.