Na Mwandishi wetu akiwa Dar Es Salaam,
Kwa Tanzania klabu za Simba SC na Yanga ndio timu kubwa lakini kwa bahati mbaya ni timu ambazo zimekuwa hazina viwanja vyenye viwango vya kufanyia mazoezi, mara nyingi hutumia viwanja vya kukodi.
Simba SC imeanzishwa mwaka 1936 wakati Yanga SC imeanzishwa mwaka 1935, timu zote hizo zimekuwa hazina viwanja vyenye viwango, upande wa Simba SC ndoto ya kupata uwanja wao wa mazoezi tayari imetimia kwani muwekezaji wao Mohammed Dewji ‘MO’ ametangaza kuwa mwisho wa mwezi Oktoba Simba SC wataanza kutumia uwanja wao.
Hiyo ni baada ya MO Dewji kutembelea na kukagua uwanja wao wa Bunju ambao unajengwa baada ya MO kushinda zabuni ya uwekezaji, imethibitika kuwa Simba hadi sasa wamekamilisha ujenzi wao uwanja wao wa mazoezi wa nyasi bandia na nyasi za asili na watakuwa wanatumia viwanja hivyo kwa mahitaji ya mechi husika na wamekamilisha vyumba vya kubadilishia nguo katika viwanja hivyo.
Hata hivyo kukamilishwa kwa ujenzi wa uwanja huo kutaisaidia Simba SC kuokoa gharama za kulipia viwanja vya kukodi kama Gymkhana, Simba SC ilikuwa inaingia gharama ya kukodi uwanja kwa saa 1 Tsh 500000/= ($240).