Rais wa Shirikisho la soka duniani FIFA aliyesimamishwa kazi kwa tuhma za ufisadi, Sepp Batter amelazwa hospitali baada ya kusumbuliwa na msongo wa mawazo.
Msemaji wake Klaus Stoehlker amethibitisha kulazwa kwa Blatter na kuongeza kuwa anatarajiwa kuruhusiwa na kwenda nyumbani mapema juma lijalo.
Aidha, Stoehlker amesema Blatter mwenye umri wa miaka 79 ameendelea kusisitiza kupigania haki yake na kushtumu Kamati ya nidhamu ya FIFA kwa kumchukulia hatua ya kumsimamisha kazi kwa siku tisini hata bila ya kumsikiliza.
Binti wa Blatter Corinne amesema baba yake ameacha kukutana na watu hadi tarehe 15 mwezi Novemba ili kumpa nafasi ya kupata nafuu haraka.
Msemaji wa Blatter anasema masaibu yaliyompata katika siku za hivi karibuni yamemsababishia msongo huo wa mawazo huku akisisitiza kuwa hana kosa.
Sepp Blatter amekuwa akiongoza FIFA tangu mwaka 1998 na miezi kadhaa iliyopita alitangaza kuwa atajiuzulu na tayari ameitisha uchaguzi mpya kufanyika tarehe 26 mwezi Februari mwaka ujao wa 2016.