Mechi namba 95 (Mbeya City 1 vs Kagera Sugar 1). Klabu ya Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 1, 2018 jijini Mbeya, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu.
Kamati iliiagiza Sekretarieti ya Bodi ya Ligi kutoa waraka kwa wamiliki wa viwanja kuhakikisha timu zinaingia uwanjani kwa kutumia milango rasmi tu.
Mechi namba 100 (Tanzania Prisons 3 vs Mbeya City 2). Kocha wa Mbeya City, Ramadhani Mwazurimo amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano), adhabu ambayo imezingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Kocha Mwazurimo aliondolewa kwenye benchi (ordered off) na Mwamuzi baada ya kumtolea lugha ya kashfa katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 14, 2018 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Pia klabu ya Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwa madai alikataa kutoa penalti kwa timu hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Kamati imeteua wajumbe watatu kupitia mkanda wa mechi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine itachunguza kiwango cha uchezeshaji cha Mwamuzi wa mechi hiyo, Bw. Israel Nkongo na kuwasilisha taarifa yake kwa ajili ya hatua zaidi.
Mechi namba 103 (Majimaji 1 vs Azam 1). Klabu ya Azam FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kukataa wachezaji wake wakaguliwe ndani kwa madai kuwa chumba kimepuliziwa dawa katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 18, 2018 Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Kitendo cha timu hiyo ni kinyume na Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu dhidi yao imezingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu. Pia klabu hiyo imeandikiwa barua ya kutakiwa kuthibitisha madai yake kuwa chumba hicho kilikuwa kimepuliziwa dawa.
Mechi namba 104 (Simba 4 vs Singida United 0).Mtunza Vifaa wa Singida United FC, Mussa Rajab amefungiwa mwezi mmoja na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kutokana na kuingia uwanjani baada ya filimbi ya mapumziko na kumlalamikia mwamuzi.
Kitendo alichofanya Mtunza Vifaa huyo katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 18, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kimekiuka Kanuni ya 14(10) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 41(2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Viongozi.
Mechi namba 106 (Mbao 0 vs Stand United 1). Klabu ya Stand United imepewa Onyo Kali kutokana na timu yake kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) kwa dakika sita, na pia kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika tisa katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 20, 2018 Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.Adhabu kwa klabu hiyo iliyokiuka Kanuni ya 14(2a) ya Ligi Kuu, imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 112 (Kagera Sugar 0 vs Simba 2). Suala la mchezaji wa Kagera Sugar, Juma Nyoso kumpiga shabiki baada ya mechi hiyo iliyochezwa Januari 22, 2018 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kumalizika, limepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 44 Kundi A (African Lyon 2 v Friends Rangers 1). Mchezaji Almasi Mkinda wa Friends Rangers amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumpiga ngumi mchezaji wa African Lyon katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 14, 2018 Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 37(3) ya Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
Nao wachezaji Mtoro Hamisi wa Friends Rangers, na Prosper Mushi wa African Lyon wamefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kila mmoja baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kupigana uwanjani. Adhabu imezingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
Daktari wa Friends Rangers, Rajabu Shabani amefungiwa miezi mitatu na kupigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kuwatolea lugha ya matusi na dharau waamuzi wa mechi hiyo. Adhabu imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Viongozi.
Klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mechi hiyo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 42(10) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 45 Kundi A (JKT Tanzania 5 v African Lyon 1). Klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kukiuka Kanuni ya 14(13) kutokana na kugoma kuingia vyumbani katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 20, 2018 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ulioko Mbweni jijini Dar es Salaam. Adhabu dhidi ya klabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Nayo JKT Tanzania imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuingia eneo la kuchezea kushangilia ushindi. Klabu hiyo imeadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 41 Kundi B (JKT Mlale 1 v Mawenzi Market 0). Daktari wa Mawenzi, Novatus Ngowi amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kuwatolea waamuzi lugha isiyokuwa ya kiungwana katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 13, 2018 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Mechi namba 43 Kundi B (Mbeya Kwanza 0 vs KMC 0). Kocha wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo iliyochezwa Januari 13, 2018 Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kumalizika akiwashambulia viongozi wa TFF akidai wanaandaa timu za kupanda Ligi Kuu, ndiyo maana waamuzi wananyonga haki yao ya kupata ushindi.
Mechi namba 47 Kundi B (Polisi Tanzania 0 vs Coastal Union 0). Klabu ya Polisi Tanzania imepigwa faini ya jumla ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na gari la washabiki wa timu hiyo kuingia uwanjani, na kuzunguka uwanja wakati timu zikifanya mazoezi. Pia wakati wa mapumziko na baada ya mchezo kumalizika washabiki wa timu hiyo waliwafuata waamuzi na kutaka kuwapiga.
Vilevile washabiki wa timu hiyo walitoa lugha chafu kwa viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA) katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 20, 2018 Uwanja wa Ushirika mjini Moshi. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mechi namba 44 Kundi C (Biashara United 2 vs Alliance Schools 0). Klabu ya Alliance Schools imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 13, 2018 katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 45 Kundi C (JKT Oljoro 1 vs Dodoma FC 1). Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Emmanuel Muga na Mwamuzi wa Akiba, Gilbyrth Mrina wamepata alama za chini hivyo kukosa sifa ya kuendelea kuchezesha Ligi.Hivyo, Kamati imeteua wajumbe watatu kupitia mkanda wa mechi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine itachunguza kiwango cha uchezeshaji cha waamuzi kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi dhidi yao.
Mechi namba 47 Kundi C (Biashara United 1 vs Rhino Rangers 1). Daktari wa Viungo wa Rhino Rangers, Ahamad Mgongo na kipa Mohamed Ibrahim Salumu wa Rhino Rangers wamesimamishwa hadi suala lao la utovu wa nidhamu waliofanya litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF. Wamesimamishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mbali ya kumpiga teke Msimamizi Msaidizi wa Kituo cha Mara, Mgongo pia wakati vurugu zikiendelea katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 21, 2018 Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma alimchapa kibao Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Athuman Rajabu.
Naye kipa Salumu baada ya kumuangusha kwa makusudi ndani ya eneo la hatari mchezaji wa Biashara United, na refa kuamuru adhabu ya penalti dhidi yake alimpiga ngumi kwa makusudi mchezaji huyo wa Biashara United. Baada ya vurugu kutulia Mwamuzi alimuonyesha kadi nyekundu. Lakini Kipa huyo baada ya kuamuliwa kutoka nje alimpiga Mwamuzi ngumi ya kisogoni.Mechi namba 48 Kundi C (Transit Camp 0 vs Alliance Schools 3). Wachezaji Mohamed Suleiman Ussi, Khalid Mahmud Konobile, Abubakar Ramadhan na Victor William Alimwene wa Transit Camp wamepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumkimbilia Mwamuzi baada ya mechi kumalizika kwa lengo la kumfanyia vurugu kabla ya askari polisi kuingilia kati.Walifanya kitendo hicho katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 21, 2018 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
LIGI DARAJA LA PILI
Mechi namba 21 Kundi C (The Mighty Elephant 2 v Burkina Faso 2).
Mchezaji Gideon Joram Richard wa The Mighty Elephant anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kitendo chake cha kwenda karibu na chumba cha waamuzi baada ya mechi na kuwakashfu kuwa ni mabwege katika mchezo huo uliofanyika Januari 15, 2018 Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
AJENDA 62/MSC/2018- MALALAMIKO YA DODOMA FC
Kamati imesikiliza malalamiko ya timu ya Dodoma FC dhidi ya JKT Oljoro katika mechi yao iliyochezwa Januari 21, 2018 kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi. Malalamiko hayo yalikuwa na sehemu mbili; moja ni uhalali wa mchezaji wa JKT Oljoro, Haki Rubea kuwa hakuwa na leseni, na mbili ni kudai kuwa Mwamuzi na Mwamuzi Msaidizi Namba Moja walikataa bao lao halali.
Baada ya kupitia malalamiko hayo, Kamati imebaini kuwa Haki Rubea ni mchezaji wa JKT Oljoro mwenye leseni namba 961111011 iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), hivyo ni mchezaji halali (qualified player). Vilevile Kamati haina mamlaka ya kukubali bao ambalo limekataliwa na Mwamuzi uwanjani. Hivyo, Kamati imetupa malalamiko ya Dodoma FC kwa hoja zote mbili.Hata hivyo, Kamati imejiridhisha kuwa Kamishna wa mechi hiyo Paul Opiyo na Mwamuzi wa Akiba, Gilbyrth Mrina walifanya makosa kumruhusu mchezaji huyo kucheza bila kuonyesha leseni yake, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(16) na 14(17) za Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Kamati imeteua wajumbe watatu kupitia mkanda wa mechi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine itachunguza kiwango cha uchezeshaji cha Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Emmanuel Muga na Mwamuzi wa Akiba, Gilbyrth Mrina na kuwasilisha taarifa yake kwa ajili ya hatua Zaidi.
Related TopicsCompetition
African journalist with passion of football reporting.Also i love politics