Klabu ya St George ya Ethiopia, APR ya Rwanda na Yanga ya Tanzania, zimefuzu katika mzunguko wa kwanza kuwania taji la klabu bingwa katika mchezo wa soka barani Afrika CAF mwaka 2016.
APR Ya Rwanda ikicheza nyumbani siku ya Jumamosi, iliishinda Mbabane Swallows wa Swaziland kwa jumla ya mabao 4 kwa 2 na sasa itamenyana na Yanga FC ya Tanzania katika mzunguko unaofuata.
Yanga nao wakicheza nyumbani katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, waliwashinda Cercle de Joachim ya Mauritania kwa jumla ya mabao 3 kwa 0, na siku ya Jumamosi ilipata ushindi wa mabao 2 kwa 0.
St. George ambayo ilitoka sare ya bao 1 kwa 1 na St Michel United ya Ushelisheli, ilifuzu kutokana na ushindi wa awali, na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4 kwa 1.
Klabu hiyo kutoka Ethiopia sasa itamenyana na mabingwa watetezi TP Mazembe ya DR Congo katika mzunguko ujao.
Matokeo mengine, CnaPS ya Madagascar iliishinda Gor Mahia ya Kenya kwa jumla ya mabao 3 kwa 1, na siku ya Jumamosi Gor wakiwa ugenini walifungwa bao 1 kwa 0.
Siku ya Jumapili, Enyimba ya Nigeria inachuana na SC Vipers ya Uganda, AS Vita Club ya DRC dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar huku Vital’O ikimenyana na Lioli ya Lesotho.
Nalo taji la Shirikisho siku ya Jumapili, Bandari FC ya Kenya itakuwa wenyeji wa FC Saint Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo jijini Nairobi.
Atletico Olympic ya Burundi, Sport Club Villa ya Uganda na JKU kutoka Zanzibar zimefuzu katika hatua ya kwanza ya michuano hiyo ya Shirikisho.