Michuano ya soka baina ya mataifa bingwa barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka katika ligi za nyumbani CHAN, imeingia siku ya pili leo Jumapili katika uwanja wa Huye mjini Butare, Kusini mwa nchi ya Rwanda.
Michuano ya kundi B, inachezwa leo na mchuano wa kwanza ulianza saa tisa mchana saa za Afrika ya Kati, baina ya Leopard Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Walia Ibex Ethiopia.
DRC imepata ushindi mkubwa wa mabao 3 kwa 0, katika mchuano ambao waliutawala vipindi vyote.
Guy Lusadisu alikuwa wa kwanza kupachika bao la kwanza katika dakika ya 45 ya mchuano huo, huku Heritier Luvumbu akifunga la pili katika dakika 47 kipindi cha pili na baadaye Meshack Elia akafunga la tatu katika dakika ya 59.
DRC ambayo ilinyakua ubingwa wa CHAN mwaka 2009 wakati michuano hii ilipozinduliwa nchini Cote D’ivoire imeshiriki katika makala yote ya michuano hii, toka mwaka 2009, 2011, 2014 na sasa 2016.
Ethiopia, ilishiriki mara ya kwanza mwaka 2014 na kuondolewa katika hatua ya makundi.
Mchuano mwingine ni kuanzia saa moja jioni kati ya Angola na Cameroon.
Mashindano haya ya CHAN yalifunguliwa jana Jumamosi, kwa michuano ya kwanza ya kundi A kupigwa katika uwanja wa Amahoro jijini Kigali.
Wenyeji Rwanda walianza vema baada ya kuwashinda Cote D’ivore bao 1 kwa 0, huku Gabon na Morroco wakitoka sare ya kutofungana.
Rwanda inaongoza kundi hilo kwa alama tatu, na sasa inasubiri mchuano dhidi ya Gabon siku ya Jumatano juma lijalo.
Gabon na Morroco zina alama moja kila mmoja katika kundi hilo.
Kesho Jumatatu, michuano ya kundi C itapigwa katika uwanja wa Nyamirambo jijini Kigali.
Mabingwa wa mwaka 2011 Tunisia watachuana na Guinea inayoshiriki katika mashindano haya kwa mara ya kwanza kuanzia saa tisa mchana, saa za Afrika ya Kati.
Nigeria nayo itamenyana na jirani yake Niger katika mchuano wa pili kuanzia saa moja jioni saa za Afrika Mashariki.
Shirikisho la soka barani Afrika katika michuano hii, inamtuza mchezaji bora wa mechi iliyochezwa.