Mabingwa watetezi wa taji la klabu bingwa barani Afrika CAF TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na AS Vita Club, vyote vimefuzu katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo baada ya kuandikisha matokeo mazuri mwishoni mwa juma lililopita.
TP Mazembe wakicheza nyumbani katika uwanja wao wa Kamalondo mjini Lubumbashi, waliwashinda Saint George ya Ethiopia bao 1 kwa 0 na kufuzu kwa jumla ya mabao 3 kwa 2 kutokana na sare ya mabao 2 kwa 2 waliyopita wiki moja iliyopita jijini Addis Ababa.
Mazembe sasa watamenyana nyumbani na ugenini na Wydad Casablanca ya Morroco katika mzunguko huu wa pili mapema mwezi Aprili na mchezo wa marudiano baadaye pia mwezi uo huo.
AS Vita Club nayo, ilifuzu kwa jumla ya mabao 2 kwa 1 baada ya kuishinda Ferroviario Maputo ya Msumbiji licha ya sare ya bao 1 kwa 1 Jumapili iliyopita lakini ushindi wa awali wa mabao 2 kwa 1 uliwasaidia kusonga mbele.
Klabu hii yenye makao yake jijini Kinshasa sasa itakutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mzunguko wa pili.
Yanga FC kutoka Tanzania pia ilifuzu na itachuana na Al-Ahly ya Misri huku Al-Merrikh ya Sudan ikipangwa kukabiliana na ES Setif ya Algeria.
Matokeo mengine na ratiba:-
Enyimba (Nigeria) vs Etoile du Sahel (Tunisia)
Stade Malien(Mali) vs Zesco United (Zambia)
ASEC Mimosas (Cote Dvoire) vs Al-Ahli Tripoli ( Libya)
Zamalek( Misri) vs Mo Bejala ( Algeria)
Taji la Shirikisho
Azam FC ya Tanzania na Sport Club Villa ya Uganda nazo zitawakilisha Afrika Mashariki katika mzunguko wa pili wa kutafuta ubingwa wa taji la Shirikisho.
Azam FC ilifuzu baada ya ushindi wa jumla ya mabao 7 kwa 3 dhidi ya Bidvest Wits ya Arfrika Kusini na sasa itakutana na Esperence de Tunis ya Tunisia katika mzunguko huu.
SC Villa nayo ilisonga mbele baada ya kuilemea JKU ya Zanzibar kwa mabao 5 kwa 0 na itakabiliana na FUS Rabat ya Morocco.
Matokeo mengine na ratiba:-
Vita Club Mokanda (Congo) vs Sagrada Esperanca (Angola)
MC Oran (Algeria) vs Kawkab Marrakech (Morroco)
Zanaco (Zambia) vs Stade Gabesien (Tunisia)
CS Constantine (Algeria) vs Misri El Makasa ( Misri)
Al-Ahly Shendi (Sudan) vs Medeama (Ghana)
CF Mounana (Gabon) vs ENPPI (Misri)