Klabu ya soka ya Etoile du Sahel kutoka Tunisia ndio mabingwa wa taji la Shirikisho barani Afrika mwaka 2015.
Sahel walikabidhiwa taji hilo baada ya kuishinda Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 2 kwa 1.
Fainali ya pili ilichezwa Jumapili jioni mwishoni mwa juma jijini Tunis na mabingwa hao kupata bao la mapema katika dakika ya 24 kipindi cha kwanza.
Ahmed Jebal ndiye alifunga bao hilo baada ya mabeki wa Orlando Pirates kujichanganya kutokana na mashambulizi kutoka kwa wapinzani wao.
Juhudi za Orlando Pirates kusawazisha bao walilofungwa ziliambulia patupu baada ya kulemewa katika safu ya kati.
Fainali ya kwanza wiki moja iliyopita, timu zote mbili zote sare ya bao 1 kwa 1 jijini Johannersburg.
Hili ni taji la pili kwa Etoile du Sahel kushinda baada ya lile la mwaka 2006 lakini mwaka 2008 ilimaliza ya pili walipokutana na watani wao CS Sfaxien pia kutoka Tunisia.
Hakuna klabu ya Afrika Kusini ambayo imewahi kushinda taji hili la Shirikisho katika historia ya mashindano haya.
Etoile du Sahel pamoja na kutuzwa kombe hilo wamejishindia pia Dola za Marekani 625 na itachuana na TP Mazembe ya DRC bingwa wa taji la klabu bingwa barani Afrika kuwania taji la Super Cup mwezi Februari mwakani.