Shirikisho la soka barani Afrika CAF, limeanza uchunguzi wa madai ya Congo Brazaville kutumia wachezaji sita wenye umri mkubwa dhidi ya Tanzania wakati wa mchezo wa mwisho kucheza fainali ya bara Afrika kwa wachezaji wasiozidi miaka 17 itakayochezwa mwezi Aprili mwaka ujao nchini Madagascar.
Congo-Brazzaville iliishinda Tanzania katika mchezo wa mzunguko wa mwisho na kufuzu katika fainali hiyo.
Baada ya kuondolewa katika michuano hiyo, Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF, liliandikia barua Shirikisho la soka barani Afrika kuchunguza umri kamili wa wachezaji hao wanaoshukiwa kuwa zaidi ya miaka 17 kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo Celestine Mwesigwa ambaye amezungumza na BBC Sport.
Tayari CAF, imetaka mchezaji mmoja Langa-Lesse Bercy kwenda jijini Cairo nchini Misri, kufanyiwa uchunguzi huo kutumia mfumo maaluma wa MRI kwa sababu Namibia ambayo pia iliondolewa katika michuano hii ililalamika kuwa mchezaji huyo alikuwa na umri mkubwa.
Kanuni za CAF zinaeleza kuwa udanganyifu wa umri ni kosa na nchi husika inaweza kupigwa marufuku ya kushiriki katika michuano ya bara Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu.
Tayari droo ya michuano hii imeshafanyika na Congo Brazaville imejumuishwa pamoja na Mali, Angola na Niger katika kundi B.