Matokeo mbalimbali yameshuhudiwa katika michuano ya klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika, iliyochezwa siku ya Jumanne na Jumatano wiki hii katika nchi mbalimbali.
Zanaco ya Zambia imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu katika hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa baada ya kuishinda Coton Sport ya Cameroon bao 1-0.
Saith Sankala aliipa klabu yake bao hilo la ushindi katika dakika ya lala salama, ya 91 ya mchuano huo uliochezwa Jumatano usiku katika uwanja wa Roumde Adjia, mjini Garaoua.
Wawakilishi hao wa Zambia wanaongoza kundi la D kwa alama 10 baada ya kushinda mechi tatu na kwenda sare mchuano mmoja.
Mabingwa wa zamani Al-Ahly ya Misri ambayo ilihitaji ushindi muhimu kufika katika hatua ya robo fainali, ilifungwa na Wydad Casablanca ya Morocco kwa mabao 2-0.
Matokeo haya yanaifanya Al-Ahly kuwa katika nafasi ya pili kwa alama 7 huku Wydad Casablanca ambayo ina nafasi ya kufuzu pia, ikiwa na alama 6 lakini Coton Sport haina alama yoyote.
Esperance de Tunis ya Tunisia, inaongoza kundi la C kwa alama 8 baada ya kutofungana na mabingwa watetezi Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
AS Vita Club ilipata ushindi wake wa kwanza baada ya kuifunga Saint George ya Ethiopia mabao 2-1.
USM Alger ya Algeria na Al-Ahli Tripoli ya Libya zinatoshana kwa alama 7 katika kundi B, baada ya mechi za wiki hii.
Al-Ahli Tripoli ikicheza nchini Tunisia kwa sababu za kiusalama, iliishinda CAPS United mabao 4-2, huku mshambuliaji wake Saleh Taher akiifungia timu yake mabao 2.
USM Alger nao wakiwa nyumbani waliifunga Zamalek mabao 2-0 jijini Algiers.
Etoile du Sahel ya Tunisia, nayo imejitengezea mazingira mazuri katika kundi A licha ya kutoka sare ya bao 1-1 na Al-Hilal ya Sudan.
Hata hivyo, ushindani mkali unatarajiwa katika kundi hili kutafuta timu mbili itakayofuzu katika hatua ya mwondoano.
Al-Merrikh ya Sudan ikicheza katika uwanja wake wa nyumbani mjini Omburman, iliishinda Ferroviario Beira ya Msumbiji mabao 2-1. Timu zote katika kundi hili lina alama nne.
Mabingwa watetezi wa taji la Shirikisho, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haikufungana na SuperSport United ya Afrika Kusini huku Horoya ya Guinea ikiishinda bao 1-0 CF Mounana ya Gabon.
Horoya inaongoza kundi hili la D kwa alama nane, ikifuatwa na Supersport United kwa alama sita sawa na TP Mazembe. CF Mounana haina alama yoyote.
Recreativo do Libolo ya Angola iliishinda Zesco ya Zambia mabao 3-0 huku Al-Hilal ya Sudan ikaifunga mabao 2-1 Smouha ya Misri, na sasa inaongoza kundi la C kwa alama 7. ZESCO United na Recretivo do Libolo zina alama sita.
MC Alger inafukuzana na CS Sfaxien katika kundi la B baada ya mzunguko wa nne wa michuano hii ya makundi. MC Alger inayoongoza kundi hilo kwa alama nane, ilishinda Mbabane Swallows mabao 2-1, huku Platinum Stars na CS Sfaxien ilitoka sare ya bao 1-1.
Ushindani mkubwa hata hivyo upo katika kundi A, FUS Rabat (Morocco), Club Africain(Tunisia) , Rivers United (Nigeria) na KCCA (Uganda) zina alama sita hadi sasa. Hii inamaanisha kuwa timu zote zipo katika nafasi nzuri ya kufuzu katika hatua ya robo fainali.
Siku ya Jumanne, Rivers United ilishinda KCCA kwa mabao 2-1 sawa na Club Africain iliyoishinda FUS Rabat pia kwa ushindi wa mabao 2-1.
Mzunguko wa tano wa michuano hii, itachezwa mwishoni mwa mwezi Juni.