Klabu ya Al-Ahly ya Misri, itachuana na ES Setif ya Algeria katika hatua ya nusu fainali kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika.
Mechi ya kwanza itachezwa tarehe 2 huku ya marudiano ikichezwa tarehe 23 mwezi Oktoba. Mechi hizi zinachezwa nyumbani na ugenini.
Al-Ahly ilifuzu katika hatua hiyo baada ya kuifunga Horoya ya Guinea mabao 4-0 baada ya mchuano wa mzunguko wa mwisho, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Nayo Primero de Agosto ya Angola itapambana na Esperance de Tunis, katika mechi nyingine ya nusu fainali.
Esperance de Tunis, ilifuzu baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 baada ya mechi ya nyumbani na ugenini dhidi ya Etoile du Sahel ya Morocco, mwishoni mwa wiki.
Primero de Agosto, iliweka historia kwa kuwa timu ya kwanza kufuzu hatua hiyo kwa faida ya bao la ugenini dhidi ya TP Mazembe ya DRC baada timu zote kutoka sare ya bao 1-1.
Katika taji la kuwania taji la Shirikisho, Enyimba ya Nigeria itamenyanana Raja Casablanca ya Morocco, huku Al-Masry ya Misri ikipangwa kucheza na AS Vita Ckub ya DRC.
Enyimba ilipata ushindi mkubwa baada ya kuishinda Rayon Sport ya Rwanda mabao 5-1, katika mechi yake ya nyumbani baada ya kutofungana jijini Kigali.
AS Vita Club nayo ilipata ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya RS Berkane baada ya kumaliza mechi yake ya ugenini.
Mechi za nusu fainali zitachezwa pia mwezi Oktoba.