Mzunguko wa pili wa michuano ya kufuzu katika hatua ya nusu fainali kuwania taji la Klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika, inachezwa mwishoni mwa juma hili.
Tayari FUS Rabat ya Morocco imefuzu katika hatua ya nusu fainali kuwania taji la Shirikisho baada ya kuishinda CS Sfaxien ya Tunisia kwa mabao 5-4 kupitia mikwaju ya penalti.
Mechi hii ilichezwa Ijumaa usiku, na baada ya kumalizika kwa sare ya bao 1-1 baada ya CS Sfaxien kufunga nyumbani baada ya kupoteza kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza, ililazimu timu zote mbili kwenda katika hatua ya penalti.
FUR Rabat imekuwa klabu ya kwanza kufuzu na sasa inasubiri mshindi kati ya Al-Hilal Al-Ubayyid ya Sudan dhidi ya mabingwa watetezi wa taji hili TP Mazembe.
Mechi hiyo muhimu itachezwa Jumapili katika uwanja wa Kamalondo mjini Lubumbashi, baada ya Mazembe kushinda mechi ya kwanza wiki iliyopita kwa mabao 2-1.
MC Alger ya Algeria itakuwa ugenini nchini Tunisia kupambana na Club Africain baada ya kushinda mechi ya wiki iliyopita kwa bao 1-0.
Mshindi wa mchuano huo atamenyana na Supersport United ya Afrika Kusini na ZESCO United wanaocheza siku ya Jumamosi.
Kuhusu michuano ya klabu bingwa, Al-Ahli Tripoli itakuwa ugenini kupambana na Etoile du Sahel siku ya Jumapili, baada ya kutofungana katika mchuano wa kwanza.
Siku ya Jumamosi, Esperance de Tunis ya Tunisia itakuwa nyumbani kucheza na Al-Ahly ya Misri baada ya matokeo ya sare ya mabao 2-2 wiki iliyopita.
Kibarua kizito kinaisubiri USM Alger ya Algeria itakayoikaribisha Ferroviario Beira ya Msumbiji, timu zote zilizotoka sare kwa kufungana bao 1-1.
Mabingwa watetezi Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusni itakuwa ugenini kujaribu kufuzu katika hatua nusu fainali kwa kuifunga Wydad Casablanca ya Morocco.
Mchuano wa kwanza wiki iliyopita, Mamelodi walishinda bao 1-0.
Michuano ya nusu fainali nyumbani na ugenini itachezwa mwisho wa mwezi huu na mwanzoni mwa mwezi Oktoba.