Timu za soka za Etoile du Sahel ya Tunisia, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kisdemokrasia ya Congo, MO Bejaia ya Algeria na FUS Rabat ya Morroco zimefuzu katika hatua ya nusu fainali kuwania taji la Shirikisho barani Afrika.
Hatua hii inakuja baada ya ya kumalizika kwa mechi za hatua ya makundi siku ya Jumanne.
Mazembe wakicheza nyumbani mjini Lubumbashi, waliwafunga Yanga FC ya Tanzania mabao 3-1 na kumaliza kundi la A kwa alama 13.
Ilikuwa bahati mbaya kwa Medeama FC ya Ghana baada ya kupoteza ugenini bao 1-0 dhidi ya MO Bejaia iliyofuzu kwa alama nane, kwa wingi wa mabao.
FUS Rabat na Etoile du Sahel nazo zilitoka sare ya kutofungana katika mchuano wao.
Etoile du Sahel itamenyana na TP Mazembe katika hatua ya nusu fainali nyumbani na ugenini, huku MO Bejaia ikipambana na FUS Rabat mwezi Septemba.
Katika michuano ya klabu bingwa, Zamalek ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini zinasubiri wapinzani wao katika hatua hii ya nusu fainali baada ya mechi ya Jumatano.
ASEC Mimosas ya Ivory Coast inacheza na Al Ahly ya Misri, zote ambazo zimeshaondolewa huku ZESCO ya Zambia ikichuana na Wydad Casablanca ya Morroco.
Zamelek itacheza na mshindi wa kundi A, ZESCO au Wydad Casablanca huku Mamelodi Sundowns ikimsubiri mshindi wa pili katika kundi hilo.