Michuano ya soka, mzunguko wa kwanza hatua ya nusu fainali kuwania taji la klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika inachezwa mwishoni mwa juma hili.
Klabu kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mabingwa wa mwaka 2010 TP Mazembe wataanza wakiwa ugenini siku ya Jumamosi kumenyana na Al-Merrikh ya Sudan jijini Khartoum. Diego Garzitto kocha wa Al-Merrikh ambaye pia aliwahi kuwa kocha wa TP Mazembe kati ya mwaka 2003 na 2004 na mwaka 2009 na 2010 amesema kuwa hana wasiwasi kuhusu mchuano huu ambao ana uhakika wa kupata ushindi nyumbani. Garzitto amesema, “ Kama mnavyojua niliwahi kuwa kocha wa TP Mazembe na nawafahamu sana wachezaji wengi na hiyo ni kazi nyespesi kwangu,”. “Kikubwa tutakachokifanya ni kufanya mashambulizi hapa nyumbani na ugenini ili kupata mabao kama tulivyofanya wakati wa mchuano dhidi ya Esperance na Kabuscorp katika hatua ya mwondoano,” alisisitiza kocha Garzitto. Al Merrikh ilifuzu baada ya kumaliza ya pili katika kundi lao nyuma ya USM Alger ya Algeria na inawategemea wachezaji kama Bakri 'Al Medina' Babiker, Didier Lebri na Francis Coffie wanaotarajiwa kuongoza mashambulizi dhidi ya Mazembe. Al-Merrikh mabingwa wa soka nchini Sudan mara 19 hawajawahi kushinda ubingwa wa CAF na mwaka huu wameonesha matokeo mazuri na kufika hatua hii ya nusu fainali tangu mwkaa 1975 walikofika hatua ya robo fainali ya michuano hii.
Naye kocha wa TP Mazembe Patrice Carteron anasema wachezaji wake wako tayari kuwakabili mabingwa hao wa Sudan.
TP Mazembe imeshiriki katika michuano 10 ya nusu fainali ya michuano hii ya klabu bingwa barani Afrika, na imeshinda michuano mitatu, kwenda sare mara tatu na kushindwa mara nne.
Siku ya Jumapili, klabu nyingine ya Sudan Al-Hilal itachuana na USM Alger ya Algeria katika michuano hii. Michuano ya marudiano itachezwa tarehe 3 na 4 mwezi Oktoba. Mbali na michuano ya klabu bingwa, Orlando Pirates ya Afrika Kusini nayo inaikaribisha Al-Ahly ya Misri katika mchuano wa kwanza wa hatua ya nusu fainali kuwania taji la Shirikisho. Siku ya Jumapili, Etoile du Sahel ya Tunisia itachuana na Zamalek pia ya Misri. Fainali itachezwa mjini Novemba nyumbani na ugenini.