Klabu ya soka ya Al Merreikh kutoka Sudan, imepata uongozi katika hatua ya nusu fainali kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika, baada ya kuifunga TP Mazembe mabao 2 kwa 1 katika mchuano wa mzunguko wa kwanza siku ya Jumamosi usiku jijini Khartoum.
Bao la ushindi la Al Merrikh lilitiwa kimyani na Bakri Babeker katika dakika za lala salama za mchuano huo baada ya kuonekana kuwa mchuano huo ungemalizika kwa sare ya bao 1 kwa 1.
Mapema mchezaji matata wa Al Merrikh Francis Coffie alitumia udhaifu wa mabeki wa Mazembe na kupachika bao la 1 katika dakika ya 41 .
Dakika 13 kabla ya kumalizika kwa mchuano huo, mshambuliaji wa Kimataifa kutoka Tanzania Thomas Ulimwengu aliisawazishia Mazembe kabla ya vijana wa Patrice Cateron kufungwa tena.
Ushindi wa Al Merrikh unawapa nafasi kubwa ya kufuzu katika hatua ya fainali, na sasa TP Mazembe italazimika kufunga mabao mawili zaidi ili kufuzu lakini klabu hii ya Sudan inahitaji sare kusonga mbele.
TP Mazembe itakuwa mwenyeji wa Al Merrikh katika mchuano wa marudiano tarehe 4 mwezi Oktoba jijini Lubumbashi.
Mchuano wa pili wa nusu fainali ni leo Jumapili kati ya wawakilishi wengine wa Sudan, Al-Hilal wanaowakaribisha USM Alger kutoka Algeria.
Michuano ya nusu fainali kutafuta ubingwa wa taji la Shirikisho pia inaendelea mwishoni mwa juma hili, na siku ya Jumamosi Orlando Pirates ya Afrika Kusini ilianza vizuri kwa kuwashinda Al-Ahly ya Misri bao 1 kwa 0.
Siku ya Jumapili Etoile du Sahel inaikaribisha Zamalek pia kutoka Misri.