Na Victor Abuso
TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imejiongezea matumaini ya kusonga mbele katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika CAF baada ya ushindi muhimu mwishoni mwa juma lililopita.
TP Mazembe ikiwa ugenini mjini Alexandria ilipata ushindi wa mabao 2 kwa 0 na kuwapa alama tatu muhimu katika kundi la A katika michuano ya makundi.
Klabu hiyo sasa inashikilia nafasi ya pili kwa alama 5, sawa na Al-Hilal ya Sudan ambayo pia ina alama 5.
Mazembe yenye makao yake mjini Lubumbashi kati ya michuano mitatu iliyocheza, imeshinda mchuano mmoja na kwenda sare miwili.
Mabingwa hao mara nne wa michuano hii mwaka 1967, 1968,2009 na 2010 wamekuwa wakipata matokeo mabaya katika siku za hivi karibuni na kuzua maswali kuhusu kikosi cha kocha Patrice Carteron.
Mchuano mwingine wa Mazembe utakuwa ni tarehe 8 mwezi Agosti dhidi ya Smouha ambao watarudiana mjini Lubumbashi.
Katika matokeo mengine, Moghreb Tetoun ilitoka sare ya bao 1 kwa 1 na Al -Hilal ya Sudan.
Matokeo mengine ya kutafuta ubingwa wa taji hili baada ya michuano ya juma lililopita, USM Alger ya Algeria iliishinda MC El Eulma mabao 2 kwa 1, huku ES Setif ikitoka sare ya bao 1 kwa 1 na Al-Merrikh ya Sudan.
USM Alger inaongoza kundi la B kwa alama 9, ikifuatwa na Al Merrikh kwa alama 4 sawa na ES Setif huku MC El Eulma ikiwa ya mwisho bila ya alama.
Michuano ya marudiano ni mwishoni mwa juma lijalo.