Nusu fainali ya pili ya mchezo wa soka kufuzu katika fainali ya michuano ya klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika, inachezwa mwishoni mwa juma hili siku ya Jumamosi na Jumapili.
Tukianza na taji la klabu bingwa, siku ya Jumamosi klabu ya USM Alger kutoka Algeria ni wenyeji wa Al Hilal ya Sudan jijini Algers katika mchuano .
Wenyeji wana nafasi kubwa ya kufuzu kutokana na ushindi walioupata katika mchuano wa mzunguko wa kwanza jijini Khartoum kwa kuwashinda Al Hilal mabao 2 kwa 1.
USM Alger wao wanahitaji sare tu ili kufuzu lakini Al Hilal wanahitaji kupata ushindi wa angalau mabao 2 kwa 0 ili kufuzu.
Mchuano huo utachezwa kuanzia saa nne na nusu usiku saa za Afrika Mashariki katika uwanja Stade Omar Hamadi jijini Algers.
Wachambuzi wa soka wanaona kuwa USM Alger wana nafasi kubwa ya kufuzu kutokana na ushindi wao wa ugenini lakini pia wako nyumbani na mashabiki wao ni muhimu katika mchuano kama huu.
Siku ya Jumapili, ni nusu fainali nyingine ya mzunguko wa pili itakayowakutanisha mabingwa wa mwaka 2010 TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo itakuwa nyumbani mjini Lubumbashi kumenyana na Al Merrikh ya Sudan.
Mwishoni mwa juma lililopita jijini Khartoum, Al Merrikh ikiwa nyumbani iliishinda TP Mazembe mabao 2 kwa 1 na pia inahitaji sare ili kufuzu.
Hata hivyo, wachambuzi wa soka wanaona kuwa kazi kubwa itakuwa ni kwa Al Merrikh kulinda lango lao kwa sababu Mazembe wana rekodi nzuri nyumbani na kuna uwezekano wa kupata mabao zaidi ya matatu katika mchuano huo.
Ili kusonga mbele, Mazembe wanahitaji kuwafunga wapinzani wao bao 1 kwa 0 kwa sbabau walipata bao la ugenini jijini Khartoum.
Mchuano huo utapigwa kuanzia saa 11 na nusu saa za Afrika Mashariki katika uwanja wa Stade TP Mazembe.
Wachambuzi wa soka wanaona kuwa fainali itawakutanisha USM Alger na TP Mazembe.
Mbali na michuano hii ya klabu bingwa, michuano ya kuwani taji la Shirikisho inapigwa.
Siku ya Jumamosi, Zamalek ya Misri watakuwa na kibarua kigumu kuifunga Etoile du Sahel ya Tunisia baada ya kufungwa mabao 5 kwa 1 katika nusu fainali ya kwanza juma lililopita.
Klabu nyingine ya Misri Al Ahly ambayo ilifungwa na Orlando Piates bao 1 kwa 0, itakuwa mwenyeji wa mchuano wa Jumapili na inahitaji kufunga angalau mabao 2 kwa 0 kuwa katika nafasi nzuri ya kufuzu katika hatua ya fainali.
Fainali ya klabu bingwa na Shirikisho itachezwa baadaye mwezi wa Novemba.