Shirikisho la soka barani Afrika CAF, limeahirisha ziara yake nchini Kenya kwenda kuthathmini utayari wa nchi hiyo kuandaa michuano ya CHAN baina ya wachezaji wanaocheza soka nyumbani mwaka ujao.
Ukaguzi huo ulikuwa umepangwa kufanyika siku ya Alhamisi tarehe saba mwezi huu, lakini CAF inasema kwa sababu ya mazingira ya kisiasa nchini humo, ukaguzi huo utafanyika wakati mwingine.
Hatua hii imekuja baada ya Mahakama ya Juu, Ijumaa iliyopita kufuta uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi uliopita.
Hata hivyo, CAF imemtuma Naibu rais wa Shirikisho la soka Constant Omari Selemani kuthathmini hali ya kisiasa nchini humo na kuamua mustakabali wa ukaguzi huo.
Omari ambaye pia ni rais wa soka nchini DRC anatarajiwa kuwasili jijini Nairobi Jumapili jioni na kukutana na watu mbalimbali.
Kumekuwa na mashaka ikiwa Kenya itafanikiwa kuandaa michuano hiyo kwa sababu viwanja vinaonekana kutokuwa tayari.