Uongozi wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF, unatoa mafunzo kwa maafisa wanaoshughulikia usalama wakati wa mchezo wa soka wakati wa mechi mbalimbali viwanjani barani Afrika.
Mkutano huo wa siku mbili, unaofadhiliwa pia na Shirikisho la soka duniani FIFA, chini ya Katibu Mkuu wa CAF Mouad Hajji.
Hajji amesema mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wakati wa michuano ya soka na kuwalinda waamuzi, wachezaji na maafisa wengine wanaoshughulikia mechi muhimu.
Mafunzo haya yanafanyika wakati huu bara la Afrika likiendelea kushuhudia vurugu za mara kwa mara, hasa mashabiki na wachezaji wakihusishwa.
Mwezi Januari, klabu ya Islamilia nchini Misri, iliondolewa katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika, baada vurugu kushuhudiwa wakati ikichuana na Club Africain ya Tunisia
Mashabiki walianza kumtupia chupa za maji mwamuzi kutoka Cameron Sidi Alioumu, na kusababisha mechi hiyo kusitishwa kabla ya muda kufika mwisho.
Hali kama hiyo pia ilishuhudiwa wakati wa mechi ya nusu fainali kuwania taji la Shirikisho kati ya RS Berkane na CS Sfaxien mwezi Mei.
Tarehe 1 mwezi Februari 2012, watu 74 waliuauawa baada ya fujo kuzuka katika uwanja wa El Ahly mjini Port Said, wakati wa mechi ya ligi kuu kati ya Al Masry na Ahly.
Watu wengine 500 walijeruhiwa katika fujo hizo, baada ya maelfu ya mashabiki wa Al Masry ambao tiu yao ilikuwa imepata ushindi wa mabao 3-1 kushamulia mashabiki wa klabu ya Ahly.