Shirikisho la soka barani Afrika, limeunda kamati yenye lengo la kuja na mbinu ya kuyasaidia mataifa matano yaliyofuzu kuliwakilisha bara la Afrika katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi kujiandaa vema kuelekea michuano hiyo.
Kamati hii mpya itaongozwa na rais wa Shirikisho la soka nchini Ghana Kwesi Nyantakyi, ambaye pia ni Naibu rais wa Shirikisho hilo.
Mbali na Nyantakyi, marais wa vyama vya soka kutoka mataifa yote yaliyofuzu, pamoja na rais wa zamani wa soka nchini Zambia Kalusha Bwalya wanaunda kamati hiyo.
Kikao cha kwanza cha Kamati hii kitafanyika mwezi Desemba nchini Urusi, wakati wa droo ya michuano hiyo ya kombe la dunia.
Mataifa ya Afrika yaliyofuzu ni pamoja na Misri, Morocco, Nigeria, Senegal na Tunisia.