Michuano ya soka ya klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika hatua ya makundi, inaendelea leo katika viwanja mbalimbali barani Afrika.
Wydad Casablanca ya Morocco inapambana na Zesco United ya Zambia katika mchuano wa Kundi A, katika michuano ya klabu bingwa.
Zesco United wanacheza ugenini baada ya kuanza vema kampeni yao kwa kuwashinda mabingwa wa zamani Al Ahly ya Misri katika mchuano wa kwanza mapema mwezi huu mjini Ndola nchini Zambia.
Wydad Casablanca ambayo ilishinda mechi yake ya kwanza dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast, inatarajiwa kutumia vema uwanja wake wa nyumbani kuendeleza ushindi wake.
Hadi sasa, vlabu vya Wyadad Casablanca, Zesco United na ASES Mimosas zina alama 3 na siku ya Jumatatu, ASES Mimosaa walishinda mechi yake dhidi ya mabingwa wa zamani Al-Ahly kwa mabao 2 kwa 1.
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini nao wako nyumbani kumenyana na Enyimba ya Nigeria katika mechi za kundi B.
Klabu hii ya Afrika Kusini itakuwa inasaka ushindi wa pili leo baada ya ushindi wake wa kwanza kutupiliwa mbali baada ya ES Setif ya Algeria kuondolewa katika michuano hii kwa kuzua fujo uwanjani.
Zamalek inaongoza kundi hili kwa alama, baada ya kushinda Enyimba katika mchuano wa kwanza bao 1 kwa 0 wiki mbili zilizopita.
Medeama FC ya Ghana, inaweka changamoto za kifedha na kushindwa mechi ya kwanza pembeni kuvaana na MO Bejaia ya Algeria katika mchuano wa pili wa kundi A, kutafuta ubingwa wa taji la Shirikisho.
Mechi ya kwanza, wawakilishi hao wa Ghana walifungwa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mabao 3 kwa 1 mjini Lubumbashi wiki mbili zilizopita.
Mechi nyingine katika kundi hili, ilichezwa jana jijini Dar es salaam wakati wawakilishi wa Tanzania Yanga FC walipofungwa na TP Mazembe kwa bao 1 kwa 0.
Yanga imepoteza mechi zake mbili ilizocheza katika hatua hii ya makundi na ni ya mwisho bila ya alama yoyote.
Etoile du Sahel ya Tunisia nayo iko nyumbani kupambana na FUS Rabat ya Morocco katika mchuano wake wa pili wa kundi B.
FUS Rabat ilianza kwa ushindi katika kundi hili, huku Etole du Sahel ikifungwa.
Jana, klabu nyingine ya Morocco Kawkab Marrakech ikiwa ugenini iliishinda Al-Ahli Tripoli ya Libya abao 2 kwa 1 na inaongoza kundi hili kwa alama 6.
Mechi zijazo zitachezwa katikati ya mwezi Julai.