Na Victor Abuso
Michuano ya marudiano mzunguko wa tatu kufuzu katika fainali za mataifa bingwa barani Afrika baina ya wachezaji wasiozidi miaka 23 inapigwa mwishoni mwa hili katika nchi mbalimbali barani Afrika.
Uganda inamenyana na Misri Jumamosi hii jijini Kampala, na wana kazi kubwa baada ya kufungwa mabao 4 kwa 0 katika mchuano wa ugenini.
Vijana wa Uganda wanahitaji ushindi wa mabao 5 kwa 0 ili kufuzu katika fainali hizo zitakazopigwa nchini Senegal kati ya tarehe 28 mwezi Novemba hadi tarehe 12 Desemba.
Michuano hiyo pia itatumiwa kutafuta timu tatu za kwanza kufuzu katika michezo ya msimu joto ya Olimpiki itakayofanyika nchini Brazil mwaka ujao.
Mataifa manane yatashiriki katika michuano hii.
Michuano mingine ya kufuzu ni kati ya Congo Brazaville itakuwa nyumbani kumenyana na Nigeria, ambayo iliishinda mabao 2 kwa 1.
Gabon ambayo ilifungwa na Mali bao 1 kwa 0, itakuwa ugenini kumenyana na Mali katika uwanja wa Stade Modibo Keita jijini Bamako.
Mchuano mwingine mgumu siku ya Jumamosi ni kati ya Zambia na Cote Dvoire, baada ya mchuano wa kwanza kumalizika kwa sare ya kutofungana jijini Abidjan.
Vijana wa Afrika Kusini wapo nyumbani kuwakaribisha Zimbabwe baada ya kutoka sare ya bao 1 kwa 1 katika mchuano wa kwanza.
Miamba wa soka Afrika Kaskazini Morroco na Tunisia nao watamenyana siku ya Jumapili baada ya Morroco kuibuka na ushindi wa bao 1 kwa 0 katika mchuano wa mzunguko wa kwanza.