Timu ya taifa ya soka ya Cameroon ambayo imekuwa ikiliwakilisha bara la Afrika katika michuano ya kutafuta ubingwa wa dunia wa mabara, imeondolewa katika mashindano hayo yanayoendelea nchini Urusi.
Mabingwa hao wa Afrika, walimaliza mechi za kundi B bila ya ushindi wowote baada ya kufungwa na Ujerumani mabao 3-1.
Cameroon illianza vibaya mashindano haya kwa kufungwa na Chile mabao 2-0, lakini ikalazimisha sare ya 1-1 na Australia.
Ujerumani ilipata mabao yake kupitia wachezaji wake Kerem Demirbay na Timo Werner aliyefunga mabao mawili.
Mshambuliaji wa Cameroon Vincent Aboubakar, alijitahidi kushambulia lango la Ujerumani na kubahatika kupata bao dakika ya 78, alipopata bao la kufuta machozi.
Haya ni matokeo mabaya kwa Cameroon katika michuano hii. Mwaka 2003, ilifika katika hatua ya fainali na kufungwa na Ufaransa bao 1-0.
Mbali na Cameroon, mataifa mengine ya Afrika ambayo yamewahi kucheza katika michuano hii iliyoanza mwaka 1992, ni pamoja na Ivory Coast (1992), Nigeria (1996) na Afrika Kusini mwaka 2009.
Michuano hii hufanyika mwaka mmoja kabla ya michuano ya kombe la dunia.