Ni rasmi sasa kuwa nchi ya Cameroon, haitakuwa mwenyeji wa fainali ya kombe la mataifa bingwa barani Afrika katika mchezo wa soka mwaka 2019.
Uamuzi huu, umefikiwa baada ya mkutano Mkuu wa wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la soka barani Afrika CAF, waliokutana siku ya Ijumaa, jijini Accra nchini Ghana.
Wakaguzi wa CAF, walizuru Cameroon na kubaini kuwa, maaandalizi yalikuwa yanakwenda taratibu sana, huku suala la usalama likiendelea kuwa tata hasa katika maeneo ambayo watu wanazungumza lugha ya Kiingereza.
Wakaguzi wa CAF walikuwa nchini Cameroon kwa ukaguzi wa mwisho kati ya Novemba tarehe 11-15.
Uongozi wa soka barani Afrika sasa, utaomba nchi inayotaka kuandaa mashindano haya, kuwasilisha maombi ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo, itakayoanza tarehe 15 mwezi Juni na kumalizika tarehe 13 mwezi Julai na kuhusisha nchi 24.
Mwenyeji mpya wa mashindano haya atatajwa tarehe 31 mwezi huu wa Desemba.
Afrika Kusini, Misri na Morocco zinapewa nafasi kubwa ya kuwania nafasi hiyo.