Timu ya taifa ya soka ya Cameroon itamenyana na Nigeria baadaye Jumatatu jioni katika mechi muhimu ya kufuzu kucheza fainali ya kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Mchuano huu unachezwa jijini Yaounde. Wiki iliyopita, wakiwa ugenini, Cameroon walifungwa mabao 4-0 na wenyeji wao Nigeria.
Kuelekea katika mchuano huu, kocha wa Cameroon Hugo Broos ameonekana kukata tamaa na kusema kuwa hakuna matumaini ya kufuzu katika fainali hiyo.
Broos amesema vijana wake watajitahidi sana kucheza vema ili kulinda heshima yao nyumbani lakini sio kufuzu katika michuano hiyo.
“Mechi hii sio muhimu kwetu ili kufuzu kucheza kombe la dunia lakini tunachotaka ni kulinda heshima yetu,” alisema.
Ikiwa Cameroon inataka kufuzu itabidi ishinde mechi zake zote tatu zinazosalia na kuomba kuwa Nigeria nayo ipoteza mechi zote zinasalia, kitu ambacho hakitawezekana.
Nigeria wanaongoza kundi la B kwa alama 7 baada ya mechi tatu, Zambia ikiwa ya pili kwa alama 4 huku Cameroon ikiwa ya tatu kwa alama 3 huku Libya Algeria ikiwa ya mwisho kwa alama 1.
Ratiba kamili, Jumatatu Septemba 4 2017
Cameroon v Nigeria
Libya v Guinea
Ratiba, Jumanne Septemba 5 2017
Congo v Ghana
Afrika Kusini v Cape Verde
Cote d’Ivoire v Gabon
DR Congo v Tunisia
Misri v Uganda
Burkina Faso v Senegal
Mali v Morocco
Algeria v Zambia